KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

SILAHA YA MWANADAMU DHIDI YA ADUI YAKE SHETANI

Zimo ndani ya mwanadamu katika nguvu hizi, nguvu mbili za nje ambazo ni "akili na utashi". Akili ndiyo nguvu dirikishi ambayo kupitia kwayo mwanadamu anaweza kudiriki/kutambua na kufahamu. Na kupambanua kheri kutokana na shari, chenye manufaa kutokana na chenye kudhuru. Na utashi ndio nguvu hifadhi ambayo kupitia kwayo, mwanadamu anaweza kuzidhibiti harakati zake na tuo zake. Basi hawezi kwenda au kukaa, kutenda wala kuacha, kunena wala kupiga kimya ila kwa muongozo wa akili na si kwa kusukumwa na maumbile.

 

Mwanadamu basi, kupitia/kwa msaada wa nguvu mbili hizi si mtumwa wa maumbile yake, bali yeye ni mfalme/mtawala wake. Anayatawala na wala hayamtawali, anayaelekeza na wala hayamuelekezi. Na hii ndio tofauti pekee baina yake na hayawani wengine. Na kwa kiwango/kiasi ambacho mwanadamu atazitumia vema nguvu zake mbili hizi, ndio huwa tofauti baina yake na hayawani wengine.

Haya, ukiongezea na nguvu ya tatu ambayo kwayo Allah amemtukuza na kumtofautisha na viumbe vyake vingine, nayo ni "dhamira". Hii ni nguvu yenye umuhimu wake baina ya nguvu za mwanadamu, kwa kuwa yenyewe ni nguvu khiyarishi. Ambayo daima huongozea kwenye kheri na kukanya shari na kumdhibiti mwanadamu katika hali zake zote na kumchunga chunga katika kila matendo yake. Na humpelekea kujuta pale atakapo tumbukia katika madhambi na huenda mbali katika kumlaumu na kumliza atakapo topea kwenye upotofu. Na ni mara chache mno mwanadamu kutokuwa na pepesi za dhamira vyovyote itakavyo kuwa tabia yake.

Basi nguvu tatu hizi, hakika si vinginevyo ndizo ngome ambazo kwazo Allah amemuhifadhi mwanadamu dhidi ya adui yake shetani. Akili kwa idiraki yake hupambanua baina ya kheri na shari na dhamira kwa uhisi wake husukumia kwenye kheri na kukataza shari. Na Iraada (utashi) kwa nguvu yake, hutenda au huacha kwa mujibu wa inavyo elekezwa na akili na dhamira. Na zote tatu hizi, ni nguvu khiyarishi na wala hapana shaka kwamba hizo ni silaha kali, mwanadamu anaweza kwa msaada wake kuyatawala maumbile yake. Na kuyaratibia mfumo ambao yataufuata ili yaweze kutekeleza kazi/majukumu yake kwa njia bora kabisa. Kama ambavyo mambo matatu hayo ni mbawa zenye nguvu ambazo kwazo anaweza kujiambatisha katika anga la mbingu. Na wala hatukusudii kwa neno "mbingu" zile nyota na sayari, wala ile rangi ya samawi iliyo juu yetu. Hakika si vinginevyo, tunalenga kwa neno hilo "mbingu" kila upeo miongoni mwa peo za utukufu kuelekea kwenye mifano ya juu. Na kila maana tukufu miongoni mwa maana za kheri na kila tabia njema inayo mvika mtu mmoja mmoja na jamii roho ya mafanikio. Yaani ukweli na utekelezaji wake, uadilifu na uaminifu, mahaba na ikhlasi, murua na ushujaa. Kujitoa muhanga na kuwapendelea kheri wengine, huruma na upole, usamehevu na ihsani. Na baki ya hizo miongoni mwa kila maana tukufu inayo stareheka kwayo nafsi na dhamira ikatua kwayo.

 

VII.   Mwanadamu atiishiwa asili/maumbile na yaandaliwa kwa manufaa yake.

            Hivi ndivyo ambavyo Allah alivyo muumba mwanadamu, hakuyafanya maisha yake kuwa ya kimaada tupu kama yalivyo maisha ya hayawani wengine. Na wala hakuyaacha kuwa ya kiroho tupu kama yalivyo maisha ya malaika. Bali aliyafanya mchanganyiko utokanao na maada na roho, ili uwepo wake kwa janibu ya kimaada uende sawa na tabia/asili ya ardhi ambayo juu yake kinahuika kiwiliwili chake. Na kwa janibu ya kiroho urandane na tabia/maumbile ya mbingu ambako huko roho yake hukimbilia. Basi kwa janibu ya ubinadamu wake akawa anao upande wa kiroho, unao mletea khususi zote za maisha matukufu. Na unamfanyia yeye katika tabia/maumbile yakechanzo cha ufahamu wa kheri na sifa tukufu.

Na zama ulipo kuwa ukhalifa medani yake ni ardhi, Allah akamtiishia mwanadamu kila kilichomo humo. Na kila kinacho izunguka miongoni mwa mbingu, jua, mwezi, sayari, nyota, pepo na mawingu yanayo amrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi. Ili aweze kuvitumia vipawa vyake katika kugundua siri zake na kuzitoa khazina zake na kuzihodhi kheri (manufaa) zake. Na aishi humo akiwa bwana mtukufu, anaye simamisha haki na uadilifu katika pande zake zote na aeneze kheri na salama mwote. Na afute jeuri, audui na dhulma na atekeleze humo kwa niaba ya Allah kila alitakalo kwa waja wake; katika amani, utulivu na salama: "ALLAH NDIYE ALIYE ZIUMBA MBINGU NA ARDHI, NA AKATEREMSHA MAJI KUTOKA MBINGUNI. NA KWA HAYO AKATOA MATUNDA KUWA NI RIZIKI YENU. NA AKAFANYA YAKUTUMIKIENI MAJAHAZI YANAYO PITA BAHARINI KWA AMRI YAKE, NA AKAIFANYA MITO IKUTUMIKIENI. NA AKALIFANYA JUA NA MWEZI KWA MANUFAA YENU DAIMA DAWAMU, NA AKAUFANYA USIKU NA MCHANA KWA MANUFAA YENU. NA AKAKUPENI KILA MLICHO MUOMBA. NA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH HAMWEZI KUZIDHIBITI..." [14:32-34] "KWANI HAMWONI YA KWAMBA ALLAH AMEVIFANYA VIKUTUMIKIENI VILIOMO MBINGUNI NA KWENYE ARDHI, NA AKAKUJAZILIENI NEEMA ZAKE, ZA DHAAHIRI NA ZA SIRI?..." [31:20]

 

VIII.    Vipawa vya mwanadamu vyatosha kabisa kumuwezesha kutekeleza vema wajibu wake.

         Utafahamikiwa kuwa Allah Ataadhamiaye hakumuacha mwanadamu mtupu hivi hivi na wala hakumshusha ardhini akiwa bila ya silaha. Bali amempa silaha kwa nguvu zote za kheri kama alivyo mpa adui yake kwa nguvu zote za shari. Na akambainishia kanuni zinazo utawala ulimwengu na kudhibiti kheri na shari zake na kuratibu manufaa na madhara yake. Na akaeneza ndani yake mwanadamu huyu siri/ajabu za fahamu na utayarifu maumbile ambao unamuwekea wazi kanuni na taratibu hizo. Na akamjaalia katika vipawa vyake nguvu inayo nasibikiana na tabia/maumbile ya kazi ya kiardhi tu. Na nguvu nyingine yenye roho ya kimungu isiyo na mahusiano na ardhi.

Basi hapana katika vipawa vya mtu chochote kinacho zidi uzito wa chembe ndogo kabisa au kinacho pungua na muktadha wa utekelezaji wa haki za ukhalifa. Ambao Allah amemuandaa kwao na akamtukuza kwa ajili yake. Basi ikiwa yeye atatekeleza wajibu wake na akaisimamia haki ya majukumu aliyo twikwa, hakika atakuwa ameifanyia insafu nafsi yake. Na atakuwa katika utukufu alio takiwa na Allah kuwa. Na ikiwa atavikusudia vipawa hivyo kuwa pumbao, malaji na matamanio, bila ya shaka atakuwa amelibadili umbile la Allah ndani yake. Na atakuwa amejitoa kwenye utukufu na kheri aliyo mtakia Allah na kuwa kama alivyo sema Atukukiaye: "NA WASOMEE KHABARI ZA YULE AMBAYE TULIMPA ISHARA (aya) ZETU, NAYE AKAJIVUA NAZO. NA SHET'ANI AKAMUANDAMA, AKAWA MIONGONI MWA WALIO POTEA. NA TUNGELI TAKA TUNGELI MTUKUZA KWA HIZO ISHARA, LAKINI YEYE ALIUSHIKILIA ULIMWENGU NA AKALIFUATA PUMBAO LAKE. BASI MFANO WAKE NI MFANO WA MBWA, UKIMUHUJUMU HUPUMUA NA KUTOA ULIMI NA UKIMWACHA PIA HUPUMUA NA KUTOA ULIMI. HUO NI MFANO WA KAUMU WANAO ZIKANUSHA ISHARA ZETU. BASI SIMULIA HADITHI, HUENDA WAKATAFAKARI. HUU NI MFANO MUOVU KABISA WA WATU WANAO KANUSHA ISHARA ZETU NA WAKAJIDHULUMU NAFSI ZAO". [7:175-177]

 

IX.     Mwanadamu ndiye mwenye jukumu la kuvitumikisha vipawa vyake:

         Allah amemsaidia mwanadamu kwa kumuumbia vipawa na kumpa nguvu zote hizi na akamuandaa ili awe mtukufu kuliko vyote kimaisha. Na awe mtukufu wao kwa daraja na muongofu wao kwa njia. Basi baada ya mwanadamu kupewa vyote hivyo, ni juu yake kurandana na vipawa vyake na kuwa kati baina ya nguvu zake, mpaka aweze kupita kwavyo katika njia ya sawa. Na kumempasa kuchunga sheria/kanuni za Allah katika ulimwengu, mpaka ajithibitishie kwa msaada wake kheri na manufaa kwa nafsi yake na wanao mzunguka. Kwani hakika Allah Ataadhamiaye ameviumba vitu vyote, kwa kheri na manufaa ya mwanadamu. Lakini yeye hakuumba kitu chenye manufaa matupu moja kwa moja wala chenye madhara matupu moja kwa moja. Bali vyote amevipa ukubali wake kwa manufaa na madhara na akakijaalia kila kitu kiasi/kiwango maalumu yanathibitika kwacho manufaa yake na yanakanushika kwacho madhara yake. Kwa hivyo basi, kitu kikitumiwa katika kilicho umbwa kwa ajili yake na kwa kiwango kilicho wekewa, huwa kitu hicho ni kheri na neema. Na kikitumiwa vibaya au kikapitilizwa kiasi chake, kitu hicho huwa shari na nakama. Na daima maisha yatokanayo na mkono wa Allah huwa sahihi yaliyo salimika na kila mapungufu, hakika si vinginevyo hufisidiwa na mkono wa mwanadamu.

Na hivi ndivyo inavyo jiri kanuni iliyo wekwa kama ilivyo bainishwa na Qur-ani Tukufu: "JEMA LILIYO KUFIKIA LIMETOKANA NA ALLAH. NA OVU LILIYO KUSIBU LINATOKANA NA NAFSI YAKO..." [4:79]  "BASI ANAYE ONGOKA ANAONGOKA KWA FAIDA YA NAFSI YAKE NA ANAYE POTEA ANAPOTEA KWA KHASARA YA NAFSI YAKE...." [10:108]

Additional information