KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UBAINIFU WA ELEWEKO NA UDHIBITI WA HUKUMU

Kadhalika katika jumla ya adabu/taratibu za midahalo/majadiliano katika Uislamu, ni kubainisha eleweko la kinacho jadiliwa na kudhibiti hukumu za mada jadiliwa. Kwani ni jambo kongamanwa baina ya watu wenye akili pevu, kwamba kuyafahamu mambo kwa ufahamu salama, huepelekea kwenye kuyatolea hukumu sahihi juu yake. Kwa sababu sehemu kubwa ya hukumu zilizo kosewa, marejeo/chanzo chake ni ule ufahamu lemavu au kukanganyika/kutatizika baina ya matamshi/maneno na maana (ya maneno hayo).

Mkanganyiko ambao hukanganyika ndani yake haki na batili na sahihi na kile kisicho sahihi. Na wanazuoni wamepata kusema: Hakika kupaacha huru mahala pa mzozo/tofauti, hupelekea ukinaifu mzuri wa hoja. Kwani matamshi pale yatakapo bainishwa maana yake na mas-ala yatakapo wekwa wazi mafuhumu (eleweko) yake, kufikia muafaka baina ya pande mbili pinzani husahalika (huwa ni kwepesi). Na rai/maoni yanayo tiwa nguvu na hoja thabiti,hudhihiri (hupata ushindi) na akili salama hutua kwenye usahihi wake.

Katika zama za karibuni, kumezuka wimbi la maudhui ya haki za walio wachache katika baadhi ya nchi. Ni jambo lisilo na ubishi kwamba ziko nchi ambazo sehemu kubwa ya wananchi wake ni Waislamu. Kama ambavyo kuna nchi ambazo asilimia kubwa ya wakazi wake, ni wale wasio Waislamu. Na pengine utakuta muislamu na asiye muislamu wote ni watu wa jinsia moja, mathalan waafrika/wazungu/waarabu na kadhalika. Isitoshe wote ni raia wa nchi moja, mathalan wote ni watanzania/waingereza/wamisri.

Swali linalo tuhusu kulijibu na ambalo mjadala wake umekithiri hivi leo, ni: Je, sheria ya Kiislamu imetofautisha katika muamala wake baina ya Waislamu na wasio Waislamu wanao ishi ndani ya nchi moja hata kama ni wachache? Yaani kwa upande wa haki na wajibu na katika nyanja za heshima ya utu na uadilifu wa kijamii.

Katika kulijibu swali hili, tunasema kutokana na ufahamu wetu wa sheria ya Kiislamu, ya kwamba sheria hii tukufu imetoa haki na wajibu sawa kwa wote. Pia ietoa haki sawa kwa wote katika nyanja za heshima ya utu, uadilifu katika masuala ya kijamii na katika kulinda maisha, mali na heshima ya kila mtu. Na katika kuyasimamisha mahusiano/mafungamano baina yao juu ya misingi ya kusameheana, kuhurumiana na katika kubadilishana manufaa aliyo yahalalisha Allah Ataadhamiaye.

Na miongoni mwa dalili/ushahidi juu ya hilo, ni kwamba sheria ya Kiislamu imewaamrisha Waislamu kujenga mahusiano yao na wasio waislamu juu ya misingi ya wema na uadilifu maadam hawajatendewa ubaya. Hebu ipe sikio la usikivu kauli hii ya Allah Ataadhamiaye: “ALLAH HAKUKATAZANI KUWAFANYIA WEMA NA UADILIFU WALE AMBAO HAWAKUKUPIGENI VITA, WALA HAWAKUKUTOENI MAKWENU. HAKIKA ALLAH HUWAPENDA WAFANYAO UADILIFU. HAKIKA ALLAH ANAKUKATAZENI KUFANYA URAFIKI NA WALE WALIO KUPIGENI VITA, NA WAKAKUTOENI MAKWENU, NA WAKASAIDIA KATIKA KUFUKUZWA KWENU. NA WANAO WAFANYA HAO MARAFIKI BASI HAO NDIO MADHAALIMU”. [60:08-09]

Yaani; Enyi wanaadamu! Allah hakukatazeni kuwapenda na kuwa na mahusiano na watu wengine mnao khitilafiana nao katika akida (itikadi) na dini. Muda wa kuwa hawa wasio Waislamu hawajakutendeeni ubaya wowote, tena ni juu yenu kuyajenga mahusiano yenu nao juu ya msingi wa wema na uadilifu. Kwa sababu Allah anawapenda wale ambao ni waadilifu katika kauli, matendo na hukumu zao. Hakika si vinginevyo, Allah anakukatazeni kuwatendea wema na kuwa na mahusiano na wale walio udhihirisha wazi uadui wao kwenu au wale wanao wasaidia maadui zenu dhidi yenu. Enyi Waislamu! Yeyote miongoni mwenu atakaye saidiana na kushirikiana na wale wanao ipiga vita dini ya Uislamu, huyo atakuwa amejiingiza mwenyewe katika kundi la madhaalimu, wanao stahiki kupata adhabu kali mno.

Ndugu msomaji wetu mwema-Allah akurehemu. Bila ya shaka utakuwa umeona na kufahamu kwamba aya mbili hizi tulizo zinukuu, zimewarasimia Waislamu kwa ufumbulizo na uwazi mkubwa. Namna ya kujenga mafungamano/mahusiano yao na wale wote wasio Waislamu, kwani aya ya kwanza inatoa wito wa kuwatendea wema na kuwa na mahusiano na wasio Waislamu ambao hawajatutendea ubaya wowote. Wakati ambapo aya ya pili inayakataza kwa wale walio tudhihirishia shari/ubaya au wanamsaidia adui yetu kutudhuru. Na hii ndio kanuni kuu enevu kwa ulingo wa kuamiliana na wote wasio Waislamu.

Ama kwa upande wa wasio Waislamu katika watu wa kitabu, ambao ni Mayahudi na Manaswara, huongezewa kwenye kanuni kuu hii, kwamba sharia ya Kiislamu imekataza kujadiliana nao ila kwa namna iliyo bora kabisa. Ili yale mahusiano mema yaliyo baina yetu yapate kuendelea. Allah Ataadhamiaye anasema: “WALA MSIJADILIANE NA WATU WA KITABU ILA KWA NJIA ILIYO NZURI KABISA, ISIPO KUWA WALE WALIO DHULUMU MIONGONI MWAO. NA SEMENI TUMEYAAMINI YALIYO TEREMSHWA KWETU NA YALIYO TEREMSHWA KWENU. NA MUNGU WETU NA MUNGU WENU NI MMOJA. NA SISI NI WENYE KUSILIMU KWAKE”. [29:46]

Na wala sharia ya Uislamu haikuishia hapo, bali imehalalisha kuliana chakula na watu wa kitabu na kula vichinjwa vyao na kuwaoa wanawake wao kinyume na wanawake wa mushrikina. Hebu isikilize pamoja nami kauli hii ya Allah Atukukiaye: “LEO MMEHALALISHIWA KILA VILIVYO VIZURI. NA CHAKULA CHA WALIO PEWA KITABU NI HALALI KWENU, NA CHAKULA CHENU NI HALALI KWAO. NA PIA WANAWAKE WEMA MIONGONI MWA WAUMINI, NA WANAWAKE WEMA MIONGONI MWA WALIO PEWA KITABU KABLA YENU, MTAKAPO WAPA MAHARI YAO, MKAFUNGA NAO NDOA, BILA YA KUFANYA UHASHARATI WALA KUWAWEKA KINYUMBA. NA ANAYE KATAA KUAMINI BILA SHAKA AMALI YAKE IMEPOTEA, NAYE KATIKA AKHERA ATAKUWA MIONGONI MWA WENYE KHASARA”. [05:05]

Na zikaja hadithi za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kufafanua yale yaliyo elezwa kwa njia ya ujumla na Qur-ani Tukufu. Zikaamrisha kuamiliana na watu wa kitabu muamala mtukufu/mwema unao simama juu ya msingi wa haki ambayo isiyo changanyika na batili. Na juu ya uadilifu ambao usio zungukwa na dhuluma na uwazi ambao usio jua unafiki au kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Na miongoni mwa hadithi hizo, ni kauli yake-Rehema na Amani zimshukie: “Yeyote atakaye mfanyia maudhi dhimiyu (asiye muislamu aliye na dhima katika dola ya Kiislamu), basi mimi ni hasimu (mgomvi) yake. Na ambaye mimi nitakuwa hasimu yake, nitahasimiana naye siku ya Kiyama”.

Na kauli yake katika hadithi nyingine: “Atakaye mfanyia maudhi dhimiyu, bila ya shaka huyo ameniudhi mimi na mwenye kuniudhi mimi, bila ya shaka huyo amemuudhi Allah”.

Waislamu na wasio waislamu watakapo kuwa wanaishi katika nchi moja na wana utaifa mmoja. Wote ni wana wa nchi moja wanao funikwa na anga moja, wanabebwa na ardhi moja na wanajumuishwa pamoja na maslahi shirika. Kama ilivyo hali hiyo hapa kwetu Tanzania na katika nyingi miongoni mwa nchi za ulimwengu huu. Tunasema: Hali itakapo kuwa hivyo, wasio waislamu wawe wachache watakavyo kuwa, watakuwa na haki sawa katika nchi yao kama walizo nazo ndugu zao waislamu. Na watakuwa na wajibu kwa nchi yao kama ule walio nao Waislamu. Na wakati huo huo kila kundi likifuata itikadi na dini yake waliyo iridhia na kujichagulia wao wenyewe. Kwa sababu itikadi (imani) na dini, hakuna kulazimishana wala kutenzana nguvu juu yake, kama alivyo sema Allah Ataadhamiaye: “HAPANA KULAZIMISHANA KATIKA DINI. KWANI UWONGOFU UMEKWISHA PAMBANUKA NA UPOTOFU. BASI ANAYE MKATAA SHET’ANI NA AKAMUAMINI ALLAH BILA YA SHAKA AMEKAMATA KISHIKO MADHUBUTI, KISICHO VUNJIKA. NA ALLAH NI MWENYE KUSIKIA, MWENYE KUJUA”. [02:256]

Na katika maana ya aya hii, zimekuja aya nyingi za Qur-ani, miongoni mwazo ni kauli yake Atukukiaye: “ANGELI TAKA MOLA WAKO MLEZI WANGELI AMINI WOTE WALIOMO KATIKA ARDHI. JE, WEWE UTAWALAZIMISHA WATU KWA NGUVU MPAKA WAWE WAUMINI? NA HAWEZI MTU KUAMINI ILA KWA IDHINI YA ALLAH. NAYE HUJAALIA ADHABU IWAFIKIE WASIO TUMIA AKILI ZAO”. [10:99-100]

Maadam asiye muislamu anaiheshimu imani ya muislamu na wala haitendei ubaya wowote na muda wa kuwa anaiheshimu haki ya uananchi (uraia) katika nchi ambayo dini yake rasmi ni Uislamu. Hapo sheria ya Uislamu inawawajibishia wafuasi na waumini wake mbadilishano wa heshima hii na inawakataza kuzifanyia utovu wa heshima imani za watu wengine. Hebu itegee sikio la uzingativu kauli yake Ataadhamiaye: “WALA MSIWATUKANE HAO WANAO WAOMBA BADALA YA ALLAH, WASIJE NAO WAKAMTUKANA ALLAH KWA JEURI BILA YA KUJUA. NAMNA HIVYO TUMEWAPAMBIA KILA UMMA VITENDO VYAO. KISHA MAREJEO YAO YATAKUWA KWA MOLA WAO MLEZI, NAYE ATAWAAMBIA WALIYO KUWA WAKIYATENDA”. [06:108]

Makala yetu yatatwawilika (yatakuwa marefu) lau tutataka kuleta mlolongo wa dalili mbali mbali ili kuthibitisha na kuonyesha kwamba sheria ya Uislamu haibagui katika suala la haki na wajibu. Na katika kutenda uadilifu baina ya watu; wakiwa ni Waislamu au sio waislamu, kwa sababu mbingu na ardhi zimesimama juu ya ubora/utukufu wa uadilifu, kama ilivyo pokewa katika hadithi tukufu. Na Allah-utakati wa mawi ni wake-amesha tuamrisha kuwa waadilifu katika kauli zetu, hukumu zetu na ushahidi wetu, tunapo utoa kwa marafiki au maadui zetu. Allah Ataadhamiaye anasema: “ENYI MLIO AMINI! KUWENI WASIMAMIZI MADHUBUTI KWA AJILI YA ALLAH MKITOA USHAHIDI KWA HAKI. WALA KUCHUKIANA NA WATU KUSIKUPELEKEENI KUTOFANYA UADILIFU. FANYENI UADILIFU. HIVYO NDIO KUWA KARIBU MNO NA UCHAMNGU. NA MCHENI ALLAH. HAKIKA ALLAH ANAZO KHABARI ZA MNAYO YATENDA”. [05:08]

Na inatutosha kutaja kisa ambacho Qur-ani Tukufu imekiashiria (imekigusia) katika aya tisa za Surat Nisaa, kuanzia aya ya 105 mpaka 113. kisa chenyewe kwa ufupi ni kwamba mtu mmoja miongoni mwa wanao udhihirisha Uislamu, akiitwa Twu’umah Bin Ab-yariq, aliiba dirii (nguo ya vita inayo valiwa kifuani ili kuzuia chomo za mikuki) ya jirani yake aitwaye Qataadah Bin Noumaan. Akaenda kuificha kwa siri kwa mtu mmoja Muyahudi aitwaye Zaid Bin Sameen. Dirii ilipo kutwa kwa Muyahudi huyo, akataja kwamba Twu’umah Bin Ab-yariq ndiye aliye kuja kuiwekesha kwake. Lakini Twu’umah akakana na kudai kwamba Muyahudi aliye kutwa na kidhibiti ndiye mwizi na wakaja ndugu za Twu’umah kumtetea. Basi ndugu msomaji wetu mwema, unafikiri ni sera ipi adilifu ambayo Qur-ani ilishuka kuitekeleza? Sera nyoofu hii ilijisawirisha katika kauli yake Allah Ataadhamiaye, tusome na tuzingatie pamoja: “HAKIKA SISI TUMEKUTEREMSHIA KITABU HIKI KWA HAKI ILI UPATE KUHUKUMU BAINA YA WATU KWA ALIVYO KUONYESHA ALLAH. WALA USIWE MTETEZI WA MAKHAAINI. NA MUOMBE MAGHFIRA ALLAH. HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA MAGHFIRA, MWENYE KUREHEMU. WALA USIWATETE WANAO KHINI NAFSI ZAO. HAKIKA ALLAH HAMPENDI ALIYE KHAAINI, MWENYE DHAMBI. WANATAKA KUJIFICHA KWA WATU, WALA HAWATAKI KUJIFICHA KWA ALLAH, NAYE YU PAMOJA NAO PALE WANAPO PANGA NJAMA USIKU KWA MANENO ASIYO YAPENDA. NA ALLAH ANAYAJUA VEMA WANAYO YATENDA”. [04:105-108]

Yaani: Hakika sisi tumekuteremshia hii Qur-ani, ewe Muhammad! Mteremsho ulio changanya pamoja haki na uadilifu, kwa lengo la kwamba upate kuwahukumu watu katika masuala yao kwa namna aliyo kufundisha Allah. Na tahadhari fikra zako zisije zikawa pamoja na wale makhaaini wanao dhihirisha kinyume na yaliyomo nyoyoni mwao. Na umuombe maghfira (msamaha) Allah kutokana na kumili moyo wako kwa mtu ambaye kutokuwa kwake na hatia hakujathibiti mbele yako. Na wala usiwatetee wale wanao zikhini nafsi zao kwa makusudi, kwani Allah hawapendi watu wenye sifa hizo. Na yule ambaye tabia yake ni kuwaonea haya watu na wala hamuonei haya Allah pamoja na kwamba Yeye anayajua fika yote wanayo yaficha na wanayo yadhihirisha.

Kisha akawasuta ndugu za Twu’umah ambao walimtetea kwa batili na wakatoa ushahidi usio adilifu, akasema Atukuakiaye: “HIVYO NYINYI MMEWATETEA HAWA KATIKA UHAI HUU WA DUNIA. BASI NANI ATAKAYE WATETEA KWA ALLAH SIKU YA KIYAMA?  AU NI NANI ATAKUWA WAKILI WAO WA KUMTEGEMEA?” [04:109]

Kisha baada ya msuto mkali huu kwa makhaaini hawa, Allah akafungua mlango wa toba ya kweli, akasema: “NA ANAYE TENDA UOVU AU AKAJIDHULUMU NAFSI YAKE, KISHA AKAOMBA MAGHFIRA KWA ALLAH, ATAMKUTA ALLAH NI MWINGI WA MAGHFIRA, MWENYE KUREHEMU”. [04:110]

Kisha akabainisha ya kwamba madhara ya matendo maovu, humrudia mtendaji wake mwenyewe, akasema: “NA ANAYE CHUMA DHAMBI, BASI AMEICHUMIA NAFSI YAKE MWENYEWE. NA ALLAH NI MJUZI, MWENYE HIKMA”. [04:111]

Kisha akawaonya wale wanao tenda matendo maovu kisha wakawabambikia (wakawasingizia) watu wasio na hatia, akawaonya kupata mwisho mbaya, akasema: “NA ATENDAYE KOSA AU DHAMBI KISHA AKAMSINGIZIA ASIYE NA KOSA, BASI AMEJITWIKA DHULMA NA DHAMBI ILIYO WAZI”. [04:112]

Kisha aya tukufu hizi zikakhitimika kwa kubainisha baadhi ya fadhila za Allah alizo mpa Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “NA LAU KUWA SI FADHILA YA ALLAH JUU YAKO NA REHEMA YAKE, KUNDI MOJA KATI YAO LINGE DHAMIRIA KUKUPOTEZA. WALA HAWAPOTEZI ILA NAFSI ZAO, WALA HAWAWEZI KUKUDHURU KWA LOLOTE. NA ALLAH AMEKUTEREMSHIA KITABU NA HIKMA NA AMEKUFUNDISHA ULIYO KUWA HUYAJUI. NA FADHILA ZA ALLAH ZILIZO JUU YAKO NI KUBWA. HAKUNA KHERI KATIKA MENGI YA WANAYO SHAURIANA KWA SIRI, ISIPO KUWA KWA YULE ANAYE AMRISHA KUTOA SADAKA, AU KUTENDA MEMA, AU KUPATANISHA BAINA YA WATU. NA MWENYE KUFANYA HAYO KWA KUTAKA RADHI YA ALLAH, BASI TUTAKUJA MPA UJIRA MKUBWA”. [04:113-114]

Kama hivi ndugu msomaji mwema, tunaziona aya tukufu hizi zinawaongozea watu kwenye haki isiyo pindishwa na matamanio/matashi nafsi wala maasi. Isiyo kengeuka kwa sababu ya upendo/chuki au kwa sababu ya wingi/uchache. Hata kama ambaye haki iko dhidi yake ni mmoja wa wale wanao dhihirisha Uislamu na wanatendewa muamala wa Waislamu, na akawa mwenye haki si katika Waislamu. Ewe msomaji mtukufu! Hebu kuwa mkweli kwa nafsi yako, je umepata kuona uadilifu unao karibiana na uadilifu huu wa Uislamu, katika utukufu, utakasifu wake na unyoofu wa sera yake?!

Additional information