KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

SIKUKUU YA EIDIL ADH-HAA NA ADABU ZAKE

 Shukrani zote ni stahiki na milki yake Allah Mtukufu, anaye waambia Waumini katika kitabu chake kitukufu: “Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako Mlezi”. Sala na salamu zimuendee mbora wa walio pata kuhiji, wanao hiji na watakao hiji mpaka siku ya Kiyama, anaye uambia umma wake: “Hakika la mwanzo tunalo anzia nalo siku yetu hii (ya Eid) ni kuswali, kisha tunarejea (majumbani mwetu) tunachinja. Basi atakaye fanya hivyo, huyo bila ya shaka ameipata Sunna yetu (amefuata mwenendo wetu). Na atakaye chinja kabla ya huko (kuswali), hakika si jenginelo, hiyo (itakuwa ni) nyama aliyo wapa watu wake wa nyumbani, haimo katika ibada ya kuchinja”. Ziwaendee kadhalika Aali, Sahaba na umati wake wote.

 Ama baadu,

 Mpendwa ndugu yetu katika Imani.

 Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

 Ni wajibu wetu kumuomba kwa unyenyekevu mkubwa Mola Muumba wetu, atuwezeshe kumshukuru sana na kwa dhati ya nafsi, nyoyo na akili zetu kwa neema hii ya kujiwa na mwezi Mtukufu wa Dhul-Hijja (Mfunguo Tatu); mmojawapo wa miezi minne mitukufu aliyo itaja Mola Mtukufu katika kitabu chake kitukufu, tusome:

 “Hakika idadi ya miezi kwa Allah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allah tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu...”. At-Tauba [09]:36

Si hivyo tu, bali ndani ya mwezi huu zimo siku kumi tukufu ambazo Allah ameziapia katika Suratul-Fajri, akasema:

Naapa kwa Alfajiri. Na kwa masiku kumi. Al-Fajri [89]:01-02

Na hivi ndivyo Mfasiri Mkuu wa Qur-ani anavyo yataja masiku hayo, tuzingatie sote:

Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hakuna amali (inayo tendwa) katika masiku (ikawa) bora kabisa kuliko (amali inayo tendwa) katika masiku kumi (ya Dhul-Hijja). Wakauliza (Maswahaba): Hata jihadi. Akajibu: Hata jihadi ila mtu aliye toka (jihadi) akiyahatarisha maisha yake na mali yake, na kisirejee kitu (yeye wala mali yake)”. Bukhaariy – Allah amrehemu.

Na imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hakuna miongoni mwa masiku yaliyo matukufu mno mbele ya Allah Mtakasifu wala amali inayo pendeza mno kwake katika (masiku) hayo, kuliko masiku kumi haya (ya Dhul-Hijja). Kwa ajili hiyo basi, kithirisheni ndani yake (kuleta) Tahalili (kusema Laa ilaaha illal-laah), Takbira (kusema Allaahu Akbar) na Tahamidi (kusema Al-hamdulillah)”. Twabaraaniy (AL-MU’UJAMUL-KABIIR]-Allah amrehemu.

Allah akurehemu-ndugu yetu katika Imani-ufahamu ya kwamba ndani ya masiku hayo kumi bora na matukufu, imo siku moja ambayo hiyo ni bora zaidi kuliko hizo nyingine. Siku hiyo tukufu na bora mno, si nyingine bali ndio ile siku ya Arafa; mwezi tisa Dhul-Hijja. Ni siku yenye fadhila adhimu, mwenye kufunga siku hiyo hulipwa ujira na thawabu maridhawa, kwani imethibiti kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema kuhusiana na kufunga siku ya Arafa: “Hufuta madhambi ya mwaka ulio pita na ujao”. Muslim-Allah amrehemu.

Ndugu wapendwa, kwa utukufu na fadhila hizo adhimu ni khasara isiyo pimika kwa muislamu kutoipania na kuipatiliza fursa hii adhimu na adimu; kwani mwaka hata mwaka ni majaaliwa yake Mola. Kuacha kutenda anuwai za amali njema katika masiku haya, ni kuikataa zawadi tuliyo pewa na Mola na hakupungui kuwa ni kuyadharau matukufu yake. Kwa hivyo basi, kila mmoja wetu ahakikishe anaitumia vema fursa hii ya upendeleo kwa kujikurubisha na kujipendekeza kwa Mola wake kupitia mlango wa ibada mbali mbali ili apate radhi, rehema na mapenzi yake Mola. Kwani ni kwa radhi, rehema na mapenzi yake Mola tu ndio mwanaadamu hunadi saada (hupata ufanisi na mafanikio) duniani na akhera.

Ndugu wasomaji wetu-Allah akurehemuni-kwa munasaba wa Eidil-Adh-haa, ndugu zenu katika Imani kupitia Mtandao wako (WEBSITE UISLAMU), tumeonelea ni vema tukaipatiliza fursa hii adhimu kukumbushana walau machache yanayo husiana na sikukuu yetu hii ambayo huja mara moja kwa mwaka. Kwa msaada wake Mola, tunasema:

Hakika hakuna awezaye kupinga ya kwamba siku ya Eid ni tunu tuliyo tunukiwa na Allah ili iwe ni siku ya furaha kwa kuvaa vizuri, kula na kunywa vilivyo vizuri na vya halali, bashasha na tabasamu kwa Waislamu wote. Ndani ya siku hiyo Waislamu hutembeleana wakapongezana kwa kuidiriki siku hii, wakapeana zawadi, wakajumuika pamoja katika anuwai za vyakula, vinywaji na baki ya tamu tamu nyingine. Wakawatembelea wagonjwa, wakawaombea kupona na kupata siha, wakawaombea walio fariki miongoni mwao, wakakusanyika pamoja katika kumdhukuru na kumtaja Mola wao, kumswalia Mtume wao, kuwaombea dua watoto wao na baki ya mambo mema mazuri.

Ni kwa ajili ya yote hayo basi, ndio wadau wa elimu (Ahlul-Ilmi) wakatongoa (wakanena): Hakika si vinginevyo, Siku ya Eid imeitwa “Eid” kwa sababu inarejea/inaleta kila mwaka furaha iliyo uhishwa (inayo onekana mpya kila mwaka).

Na ni kwa ajili hiyo basi, ndio Allah akatuwekea na kutupa Eid mbili; Eidil-Fitri (Eid ya Mfunguo Mosi) ambayo hii husherehekewa baada ya Waislamu kumaliza kutekeleza ibada ya Swaumu ya Ramadhani. Ni kwa muktadha huo basi, ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatuambia: “Anazo mfungaji furaha mbili; anapofuturu (fungua swaumu) hufurahi kwa kufungua kwake na atakapo kutana na Bwana Mlezi wake, atafurahi kwa swaumu yake (kutokana na ujira maridhawa atakao pewa)”. Bukhaariy [1904] & Muslim [1151]-Allah awarehemu.

Na Edil-Adh-haa (Eid ya kuchinja ya Mfunguo Tatu), ambayo hii husherehekewa baada ya Waislamu kukamilisha ibada tukufu ya Hija. Na huwa katika siku ile ya kuchinja ambayo ni mwezi 10 Dhul-Hijja.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo hamia Madina kutoka Makka, aliwakuta wenyeji wa huko (Waislamu wa Madina) wana siku mbili za furaha na kucheza, akawauliza: “Ni siku mbili gani hizi?” Wakamjibu: Tulikuwa tukicheza na kufurahi katika siku mbili hizo zama za Jahilia (kabla ya kuingia kwa Uislamu). Mtume akawaambia: “Hakika Allah amekubadilishieni siku hizo kwa kukupeni siku mbili zilizo bora kuliko hizo; Eidil-Fitri na Eidil-Adh-haa”. Abu Daawoud [1904], Nasaai [1556] & Ahmad [03/103]-Allah awarehemu.

Ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu-kwa kauli hiyo ya Bwana Mtume aliyo waambia Answaari bali umma wake wote pia, tutafahamu ya kwamba Eid ni malipwa na kipawa cha Mola alicho watunukia waja wake, kwa hivyo basi kinahitaji kushukuriwa. Tumshukuru Mola wetu kwa neema hii ya kutuletea siku ya Eid, na tutambue ya kwamba kushukuru hakuwi ila ni kwa kuzidi kumtii Allah; Mola Mtoa vipawa pasina kuombwa, huo ni upande mmoja. Na upande wa pili ni kwa kujiepusha na kumuasi kwa kisingizio cha kusherehekea Eid. Na ili tuweze kuisherehekea sikukuu yetu kwa namna bora, namna itakiwayo, namna itakayo tuhakikishia kupata baraka na radhi za Mola wetu, anatakikana kila mmoja wetu kuzijua adabu/taratibu za kufuata katika siku ya Eid. Zifuatazo sasa ni baadhi ya taratibu na mambo anayo paswa kuyafanya Muislamu katika siku ya Eid yake, tufuatane pamoja, tuzingatie na kisha tuyatie matendoni:

 1. Kuwa na nia njema (iliyo takasika kwa ajili ya Allah tu):

 Muislamu anatakiwa kupitia kuifurahikia na kuisherehekea kwake siku ya Eid, atie nia ya kumshukuru Allah kwa kipawa/zawadi hiyo ya Eid ili alipwe kwa kila jema atakalo jaaliwa kulitenda katika siku hiyo. Na atambue ya kwamba Allah anapenda na kufurahi mno pindi mja anapo onyesha athari ya neema alizo mpa. Na kwa swala ya Eid, anuie kuifuata Sunna ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na kwa kuwatembelea ndugu na jamaa zake, anuie kuunga udugu. Na kwa kuwapongeza ndugu, jamaa na rafiki zake, anuie kutia furaha mioyoni mwa ndugu zake Waislamu. Na kama hivyo afanye kwa kila jambo jema la kheri analo litenda, ili ahodhi ujira na thawabu maridhawa.

 

 1. Kuoga:

 Ni suna kwa Muislamu kuoga kwa ajili ya kuhudhuria swala ya Eid na hilo ni jambo lililo thibiti kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-pasina chembe ya shaka. Imepokewa kwamba mtu mmoja alimuuliza Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-kuhusiana na josho (kuoga), akamjibu: Oga kila siku ukitaka. Yule (muulizaji) akasema: Hapana (siulizii kuoga kwa ada, bali) kuoga ambako huko ni kuoga (kwa suna). Akamjibu: (Oga) siku ya Ijumaa, siku ya Arafa, siku ya kuchinja (Eidil-Adh-haa) na siku ya Fitiri (Eidil-Fitri)”. Al-Baihaqiy [SUNANUL-KUBRAA 03/278], Shaafiy [AL-MUSNAD 01/385]-Allah awarehemu.

 Na imepokewa na Naafi kwamba Ibn Umar-Allah awawiye radhi: “Alikuwa akioga siku ya Eidil-Fitri kabla hajadamkia kwenye muswala (mahala pa kuswalia) wake”. Maalik [AL-MUTWAA 01/115]-Allah amrehemu .

 Na limesuniwa josho hili, ili muislamu apate kuwa nadhifu na mwenye harufu nzuri anapokuwa miongoni mwa waislamu wenzake katika siku ya Eid, asiwakere watu kutokana na uchafu na harufu mbaya kiasi cha kuona dhiki kukaa jirani naye.

 

 1. Kuvaa nguo nzuri kabisa:

 Kumependelewa muislamu kuvaa nguo mpya anapo kwenda kuhudhuria swala ya Eid, kama ana uwezo wa hilo, la hana uwezo, basi kunamlazimu kuvaa nguo nzuri kabisa miongoni mwa alizo nazo. Kwani kumependelewa kwetu sisi kuonyesha furaha na pambo katika siku ya Eid ili watu wapate kuwaona waislamu wakiwa katika sura na mandhari nzuri katika sikukuu zao.

 Na asili/msingi wa sunna na kupendelewa huko ni ile hadithi ya Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Alitwaa Umar juba la hariri nzito lililo kuwa likiuzwa sokoni, akalinunua. Kisha akamwendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Ewe Mtume wa Allah! Litwae hili, ujipambe nalo kwa ajili ya Eid na (kuwapokea) wajumbe...”. Bukhaariy [886] & Muslim [2068]-Allah awarehemu.

 Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Siku ya Eid alikuwa akivaa burda nyekundu”. Twabaraaniy (AL-AUSATW 02/53]-Allah amrehemu.

 

 1. Kujitia (kujipaka) uturi (manukato):

 Siku ya Eid ni sunna Muislamu kujitia/kujipulizia manukato au kujifukiza udi ili apate kunukia vizuri atakapo kuwa kwenye swala pamoja na waislamu wenzake. Asimkere mtu kutokana na harufu mbaya ya mwili wake ili kila mmoja aihisi furaha ya Eid.

 

 1. Kutokula au kunywa chochote kabla ya kuswali:

 Katika Eidil-Adh-haa si sunna muislamu kula au kunywa chochote kabla ya kuswali swala ya Eid kinyume na Eidil-Fitri; anatakiwa aende kuswali bila ya kula au kunywa chochote. Baada ya swala sasa, ndio anaweza kula au kunywa.

 Imepokewa kutoka kwa Buraidah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa hatoki siku ya Eidil-Fitri mpaka ale na wala hali siku ya Eidil-Adh-haa mpaka aswali (kwanza)”. Tirmidhiy [542]-Allah amrehemu.

 

 1. Kwenda mapema kwenye swala ya Eid:

 Hili la kwenda mapema kwenye swala ya Eid ni katika Sunna yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwani yeye ndiye aliye sema katika muongozo wa swala ya Eidil-Adh-haa: “Hakika la mwanzo tunalo anza nalo siku yetu hii (ya Eid) ni kuswali, kisha tunarejea (majumbani mwetu) tunachinja. Basi atakaye fanya hivyo, huyo bila ya shaka ameipata Sunna yetu (amefuata mwenendo wetu). Na atakaye chinja kabla ya huko (kuswali), hakika si jenginelo, hiyo (itakuwa ni) nyama aliyo wapa watu wake wa nyumbani, haimo katika ibada ya kuchinja”. Bukhaariy [968] & Muslim [1961]-Allah awarehemu.

 

 1. Kwenda mahala pa kuswalia kwa miguu:

 Wako baadhi ya watu wanao kwenda mahala panapo swaliwa swala Eid kwa kutumia vipando, lakini lililo bora ni kwenda huko kwa kutembea ila tu kama patakuwa ni mbali au yeye ni mgonjwa hawezi kutembea. Basi katika hali mbili hizo; umbali na ugonjwa anaweza kupanda kipando na hana makosa.

 Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-amesema: “Ni katika Sunna kutoka kwenda kwenye muswala wa Eid kwa kutembea”. Tirmidhiy [530] & Ibn Maajah [1296]-Allah awarehemu.

 Kauli hii ya Imamu Aliy inatiliwa nguvu na hadithi iliyo pokewa na Ibn Umar-Allah awawiye radhi: “Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akitoka kwenda kwenye muswala wa Eid kwa miguu na akirudi kwa miguu”. Ibn Maajah [1295]-Allah amrehemu.

 

 1. Kwenda kwenye muswala wa Eid kwa njia moja na kurudi kwa njia nyingine:

 Kumependelewa kwa muislamu kwenda mahala inapo swaliwa swala ya Eid kwa njia moja na wakati wa kurudi nyumbani kwake abadili njia, apite njia nyingine isiyo ile aliyo pita wakati wa kuja.

 Imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Abdillah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akibadili njia katika siku ya Eid”. Bukhaariy [986]-Allah amuwiye radhi.

 Ni kwa kuizingatia hadithi hii basi, ndio Wanazuoni wengi-Allah awarehemu-wakalipendezesha jambo hili la kwenda kuswali Eid kwa njia moja na kurudi nyumbani kwa njia nyingine, kwa kumfuata na kumuiga Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Na falsafa ya kufanya hivyo huenda ikawa ni ili apate kuonana na watu wengi, wapeane pongezi na salamu za Eid na ili ipate kuenea na kuonekana furaha ya Eid kila mahala. Na si hivyo tu, bali ili muislamu apate ujira wa ziada, kwani ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba ardhi itamshuhudilia kwamba yeye alikuwa anatembea juu yake kwenda au kurudi msikitini.

 

 1. Swala ya Eid iswaliwe uwanjani; mahala pa wazi na sio msikitini:

 Leo tunawaona watu wengi wanaswali swala ya Eid misikitini na wanaacha kuswali uwanjani pasina udhuru wowote, hilo ni kosa. Kwani sunna khasa iliyo thibiti kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ni kwamba yeye alikuwa akiwakusanya watu mawandani nje ya Madina ili kuwaswalisha swala ya Eid.

 Dalili/ushahidi wa hili ni ile hadithi iliyo pokewa na Abu Saeid Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akitoka siku ya Eidil-Fitri na ya Eidil-Adh-haa kwenda kwenye muswala. Basi cha mwanzo alicho anza nacho ni swala, kisha huinuka akawaelekea watu ilhali watu wakiwa wamekaa kwenye safu zao, akawawaidhi na kuwausia...”. Bukhaariy [956] & Muslim [80]-Allah awarehemu.

 Ila tu kama kutakuwa na mvua kubwa, upepo mkali, ukosefu wa usalama au mfano wa hayo, basi hapo kutajuzu kuswalia msikitini ili kuwaondoshea madhara waislamu.

 

 1. Kuleta kwa wingi Takbira na Tahalili katika siku za Eid:

 Tambua na ufahamu ewe ndugu yetu mwema-Allah akurehemu-ya kwamba Takbira katika siku ya Eidil-Fitri, huanza tangu kuzama kwa jua la siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani mpaka baada ya kuswaliwa kwa swala ya Eid, hapo tena hukoma Takbira. Ama Takbira za Eidil-Adh-haa, hizi huanza Alfajiri ya siku ya Arafa (Mwezi 9) mpaka siku ya mwisho ya masiku ya misikita (kuanika nyama; siku tatu za baada ya Eid; mwezi 11, 12 na 13). Na hili limethibiti pasina shaka kutoka kwa Imamu Aliy, Ibn Masoud na Ibn Abbas-Allah awawiye radhi.

 Allah Mtukufu amesema kuhusiana na Takbira za Eidil-Fitri:

 “... na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Allah kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru”. Al-Baqarah [02]:185

 Ama kuhusiana na Takbira za Eidil-Adh-haa tunasoma:

 “Na mtajeni Allah katika katika zile siku zinazo hisabiwa...”. Al-Baqarah [02]:203

 Na imepokewa kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ya kwamba yeye “Alikuwa akitoka siku ya Eidil-Fitri, akileta Takbira mpaka anafika kwenye muswala na mpaka anamaliza kuswali. Na anapo maliza kuswali, hukata Takbira”. Ibn Abi Shaibah [01/487]-Allah amrehemu.

 Na imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi: “Ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akitoka katika zile siku za Eid mbili (Eidil-Fitri na Eidil-Adh-haa) akiambatana na Al-Fadhli bin Abbas, Abdullah bin Abbas na Abbas (mwenyewe; baba yao), na (Ibn Ami yake) Aliy, Ja’afar, na (wajukuu zake) Hassan na Hussein. Na Usaamah bin Zeid, Zeid bin Haarithah na Aiman bin Ummu Aiman-Allah awawiye radhi. (Akitoka nao) hali ya kupaaza (kunyanyua) sauti zao kwa kuleta Tahalili na Takbira”. Al-Baihaqiy [03/279]-Allah awawiye radhi.

 

 1. Kuruhusiwa kucheza pasina kutumbukia katika maasia:

 Uislamu ni dini inayo randana na maumbile ya mwanaadamu, ni kwa ajili hiyo basi, Uislamu umewapa ruhusa Waislamu kufurahi na kucheza katika siku za Eid ndani ya mazingira ya mipaka iliyo wekwa na Mungu. Wacheze na kufurahi muda wa kuwa ndani ya furaha zao hizo na michezo yao hiyo, hakuna lolote la maasia litakalo waletea ghadhabu na hasira ya Mola Muumba wao.

 Kwani imepokewa kutoka kwa Urwah bin Masoud, naye akipokea kutoka kwa Mama wa Waumini; Aysha-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Abubakri (baba yake) aliingia kwake (nyumbani kwa Mtume) naye (Bi. Aysha) akiwa na vijakazi wawili wakiimba na kupiga dufu na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa nyuma ya pazia. Abubakri akawakemea, Mtume akafunua pazia na akamwambia: “Waache (waendelee kuimba na kupiga dufu lao), ewe Abubakri. Kwani haya ni masiku ya Eid”.

 Na akasema (Bi. Aysha): Nilimuona Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akinisitiri kwa burda lake ilhali mimi nikiwaangalia Wahabeshi nao wakiwa wanacheza ilhali mimi (wakati huo ni) kigori, naye (Mtume) akisema: “Kadirieni kiasi cha furaha ya mwana kigori mwenye umri mdogo”. Muslim [892]-Allah amrehemu.

 

 1. Kuunga udugu:

 Kuunga udugu ni jambo la wajibu litakikanalo wakati wote, lakini limesisitizwa mno katika siku za Eid ili kutia furaha kwa ndugu, jamaa na marafiki kupitia kutembeleana, kupeana zawadi, kualikana chakula, kufanya matembezi ya halali ya pamoja na baki ya mengine yanayo leta raha na furaha moyoni.

 Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakaye pendezwa kukunjuliwa riziki yake au kubakishiwa athari (ya matendo) yake, basi na auunge udugu wake”. Bukhaariy [2067]-Allah amrehemu.

 

 1. Kujitahidi mno kufanya ibada na twaa na kujiepusha na madhambi na maasia:

 Ewe ndugu yetu mwema-Allah akurehemu-unaonaje, Allah Mola wetu Mtukufu ametutunukia neema hii ya kuidiriki siku ya Eid; siku yenye vipawa na ukarimu wake mwingi, si ni wajibu wetu kuipokea neema hii kwa kumshukuru na si kwa kumuasi?!

 Na kushukuru neema si kwa maneno, hakika kushukuru kwa kweli khasa huwa ni kwa moyo, ulimi, viungo, fikra na kila alicho nacho mtu. Na ili kuifikia shukrani ya kweli ni lazima tuzitambue neema zake Mola kwetu, tuzithamini na kuzikubali kuwa ni neema na kisha ndio tuutumie ulimi na viungo vyetu kumshukuru.

 Na ni kheri kwetu ikiwa tutatambua kwamba kila siku inayo tupitia nasi tukiwa tumo katika kumtii Mola wetu, basi tujue kuwa sisi tumo ndani ya Eid, pamesemwa na walio sema (Hakika si jinginelo, Eid ni kwa yule aliye mtii Allah). Kwa ajili hiyo basi, hatuna budi tutahadhari kutumbukia katika maasi, kupuuzia swala kwa kisingizio cha sikukuu, kwenda kwenye majumba ya sinema, watoto wa kike kurandaranda hovyo mitaani na mengineyo miongoni mwa maovu na madhambi. Tumuombe Allah kwa rehema zake atutie katika kundi la waja wake wenye kumtii na asitupe mtihani wa kuyapenda maasia.

 Ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu-kwa mwaka huu tukomee hapa, huku sote kwa pamoja tumuombe Allah atutakabalie amali zetu zote anazo tuwezesha kuzitenda ndani ya mwezi huu mtukufu ikiwa ni pamoja na vichinjwa vyetu na ajaalie amali zetu zote ziwe ni kwa ajili yake tu. Atuwezeshe kutubia kwake toba nasuha (toba ya kweli kweli), atuwezeshe kuendelea kujipinda kumuabudu katika kipindi chetu chote cha uhai ulio bakia. Awatakabalie mahujaji wetu Hija zao na ambao hatukujaaliwa kuhiji mwaka huu, kwa rehema na fadhila zake atutie katika orodha ya mahujaji wa mwakani. Atuwafikishe kuisherehekea Sikukuu ya Eid kwa namna ile anayo ipenda na kuiridhia Yeye na Mtume wake.

 

EIDIL-MUBAARAKA KWENU NYOTE!

 

 

Additional information