KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

HUKUMU YA KIPOROMOKWA NA SHAHIDI

Þ    Kiporomokwa {Siqtwu}: Huyu ni mtoto aliyezaliwa chini ya miezi sita.

 

Þ    Shahidi: Huyu ni yule aliyeuliwa na makafiri katika vita ya kuutetea na kuulinda Uislamu.

 

 A.     Kiporomokwa:

 

Huyu katika sheria ana hali mbili kama zifuatazo:-

 

 

HALI YA KWANZA: Kutokulia/kutokutoa sauti wakati wa kuzaliwa. Huyu ikiwa hakutimia umri wa miezi minne mimbani, si wajibu kumkosha, kumkafini wala kumswalia. Lakini kumesuniwa kumkafini kwa kitambaa na kumzika bila ya kumswalia.

 

 

 

HALI YA PILI: Kulia/kutoa sauti wakati wa kuzaliwa au kupatikana yakini ya uhai wake kwa kutukusika kwake wakati huo au mfano wake tendo hilo miongoni mwa matendo yanayoashiria kuwa kazaliwa akiwa hai (yaani amekufa mara tu baada ya kuzaliwa). Huyu kutawajibika kumfanyia yote anayofanyiwa maiti mtu mzima bila ya tofauti yo yote; kuanzia kuoshwa, kukafiniwa, kuswaliwa na kuzikwa.

 

Imepokewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mtoto mchanga haswaliwi, harithi na wala harithiwi mpaka atoe sauti/alie au atukusike”. Tirmidhiy [1032] & wengineo-Allah awarehemu. Pia imepokewa kutoka kwake tena amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Kiporomokwa kitakapolia/toa sauti/tukusika, kitaswaliwa na kurithi”. Ibn Maajah [1508]-Allah amrehemu.

 

 

 

B.     Shahidi:

 

Huyu hakoshwi na wala haswaliwi na kumesuniwa kumkafini kwa nguo zake zile zile alizouliwa akiwa amezivaa pamoja na damu yake. Imepokewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliamuru wauliwa (mashahidi) wa Uhud wazikwe katika damu zao (nguo walizofia) na hawakuoshwa wala kuswaliwa. Bukhaariy [1278]-Allah amrehemu. Angalia: Iwapo mujahidi atajeruhiwa vibaya vitani na akaendelea kuwa mahututi mpaka kumalizika kwa vita ndipo akafa kutokana na majeraha ya vita. Huyu hatazingatiwa kuwa shahidi kwa upande wa matendo ya kudunia, kwa hivyo atakoshwa na kuswaliwa kama ilivyo ada.

 

 

 

Falsafa/hekima ya kutokuswaliwa wala kukoshwa shahidi:

 

Shahidi hakoshwi na wala haswaliwi kwa ajili ya kumbakishia athari/alama ya kufa shahidi na kumtukuza kwa kumtoshelezea na dua za watu (swala ya jeneza). Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ninamuapia yule ambaye nafsi ya Muhammad imo mkononi mwake, hapana jeraha lo lote lililo patikana katika njia ya Allah ila litakuja (siku ya Kiyama) vile vile kama siku lilipojeruhiwa; rangi yake rangi ya damu na harufu yake harufu ya miski”. Bukhaariy [235] & Muslim [1876]-Allah awarehemu.

 

 

 

       I.          Kuzuru makaburi:

 

           Kuyazuru makaburi ya waislamu ni jambo lililosuniwa kwa wanamume kwa mujibu wa kongamano la wanavyuoni. Kongamano litokanalo na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-katika hadithi sahihi: “Nilikuwa nimekukatazeni kuzuru makaburi, basi (sasa) yazuruni”. Muslim [977]-Allah amrehemu.

 

Na katika riwaya iliyopokelewa na Imamu Tirmidhiy [1054]-Allah amrehemu-kuna ziada: “Kwani hayo (makaburi) hukumbusha akhera”. Na tayari imekwishakupitia katika darsa tangulizi hadithi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kulizuru kaburi la mama yake. Kumbuka ziara ya makaburi ni wakati wo wote; haina wakati/siku maalumu kuwa ndio inafaa zaidi kuliko wakati/siku nyingine.

 

Ama wanawake wa Kiislamu ni karaha kwao kuzuru makaburi. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-amesema: “Allah amewalaani wanawake wazuruo makaburi”. Abu Daawoud [3236]-Allah amrehemu. Lakini kumesuniwa kwao kama ilivyo kwa wanamume kulizuru kaburi la Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na makaburi ya mitume wengine na waja wema. Suna hii inaambatana na sharti ya kutoonyesha mapambo, kuchanganyika na kusongamana na wanaume na kutoinua sauti zao.

 

 

 

  VI.          Miongoni mwa adabu za ziara:

 

           Mzuruji atakapoingia katika viwanja vya makaburi, kumesuniwa kwake kuwatolea salamu maiti waliozikwa hapo kwa kusema: ASSALAAMU ALAYKUM DAARA QAUMIN MUUMINIYNA, WA INNAA INSHAALLAAHU BIKUM LAAHIQUUN”. Muslim [249]-Allah amrehemu.

 

MAANA: “Amani ikushukieni enyi nyumba ya watu waumini na hakika sisi apendapo Allah tutakutana nanyi”.

Na awasomee kitakachomuwepesikia katika Qur-ani, halafu awaombee Mungu baada ya kisomo hicho. Na azitoe hidaya thawabu za kisomo hicho kwa roho za maiti hao kwani dua hutarajiwa mno kujibiwa hapo.  Na dua ikijibiwa maiti watanufaika na thawabu za Qur-ani iliyosomwa. Allah ndiye Mjuzi mno.

Additional information