KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

WASIO WAISLAMU WAKINAISHWA NA USHINDI WA VITA HIVI

Kama vita vya Khaybar vilivyoutamatisha utawala na ukaliaji wa Mayahudi katika ardhi za Waarabu. Ndivyo hivyo hivyo vilivyoitoa jeuri na kibri cha Makureishi na kuwaacha mbele ya nguvu ya Uislamu wakiwa wametoshewa na kuhemewa. Wakiwa hawajui cha kufanya kuuelekea mwumbi huu mkokoto wa maji usioweza kuzuiwa na nguvu yo yote. Hapo ndipo Makureishi na Waarabu wote kwa ujumla wao wakalazimika kukubali na kukiri kwamba hawana tena ubavu wa kupambana na dini hii. Wakawa hawana budi kusalimu amri na kuukubali uhalisia wa hali bila ya hiari zao.

Na tangu hapo hakupatikana tena mtu wa kuupiga vita Uislamu miongoni mwa wakazi wa kisiwa cha Waarabu ila vikundi vidogo vidogo  vichache vya mabedui wa jangwani. Hawa wakawa wakilikinga wimbi hili kama linavyokingama povu katika njia ya mumbwi. Ambapo mumbwi hulifagilia mbali povu hilo na kuliacha likitawanyikia pembeni. Pakawa hapana budi kuadhibiwa wakaidi wachache hawa wanaojaribu kushindana na nguvu ya Allah isiyoshindika. Kwa ajili hii, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawa anatuma huku na huko vikosi vya askari kwa lengo la kuhakikisha amani na usalama. Na kujenga hali bora itakayowawezesha wana-da’awah (walinganiaji wa ujumbe wa Allah) kuufikisha ujumbe wa Allah pande mbalimbali bila ya bughudha au kufanyiwa khiana/usaliti.

 

BARUA KWA WAFALME

 

 

             i.          Dola za Uajemi na Urumi ndizo zilizokuwa madola makuu ya wakati huo:

 

            Muda mfupi baada ya kumalizika kwa suluhu ya Hudaybiyah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza kuwaandikia barua wafalme na watawala walio mzunguka. Madhumuni ya barua hizi za Mtume kwa wafalme hawa, ilikuwa ni kuwalingania Uislamu. Na dola kubwa za wakati huo zilikuwa ni Uajemi, Urumi na Uhabeshi. Uajemi ilikuwa ni dola ya kimajusi inayofuata itikadi ya kuabudu moto na Urumi na Uhabeshi zilikuwa ni dola zinazofuata itikadi ya Kinaswara. Palikuwa na msuguano mkali na mapambano ya mara kwa mara baina yao, na kupokezana ushindi na ushindwa. Hali iliendelea hivyo kwa miaka kadhaa mpaka pale walipofikia maafikiano ya kuweka chini silaha. Ukiachilia mbali dola tatu hizi, zilizobakia zilikuwa ni dola na himaya ndogo ndogo ambazo ama zilikuwa upande wa Uajemi au ule wa Urumi. Na nyingine zilikuwa ni dola huru; zisizojihusisha na upande wo wote. Dola za Yemen na Iraq zilikuwa chini ya uongozi wa Uajemi, Shamu na Misri zilikuwa chini ya utawala wa Urumi. Na Yamaamah, Oman na Bahrein zilikuwa ni falme huru zisizoegemea upande wo wote wa madola makuu haya.

 

Ama Tihaamah, Hijaazi, Najid na Twaif na miji iliyozizunguka katikati ya ghuba ya Kiarabu, hazikuunganishwa na madola mawili haya ila kwa mahusiano ya kibiashara tu. Lakini hisia za kidini zilikuwa zikiyafanya matamanio/mapenzi ya mushrikina kuwa pamoja na Uajemi. Na kuyafanya mapenzi ya waislamu kuwa pamoja na Warumi, kwa hivyo wote kwa pamoja; waislamu na mushrikina wakawa wakizifuatilia kwa makini na mapenzi makubwa khabari za vita baina ya madola mawili makuu haya; Urumi na Uajemi. Kila kundi likishehenezwa na mapenzi ya kutaka ushindi uwe ni fungu la washirika wao, mushrikina wote wakipenda Uajemi iwashinde Warumi. Na waislamu wakipendelea ushindi wa Warumi dhidi ya Waajemi, kwa kuwa wao ni watu wa kitabu. Mnamo mwaka 621 A.D.; mwaka mmoja tu kabla ya Hijrah, ilitokezea Waajemi; washirika wa mushrikina kuwashambulia Warumi; washirika wa waislamu na kuwashinda. Wakaendeleza wimbi hilo la ushindi mpaka wakafika ndani kabisa ya Asia ndogo na kuusambaratisha “Birantwiyah”; mji mkuu wa dola ya Urumi. Mushrikina wakafurahi mno na kuushangilia ushindi huu wa washirika wao dhidi ya washirika wa waislamu. Kwa ushindi huo, wakabashiri ushindi wa itikadi ya miungu wengi dhidi ya itikadi ya Mungu mmoja (Tauheed ya waislamu). Hapo ndipo Allah Taala alipoziteremsha aya za mwanzo za Suurat-Ruum akiwapa bishara njema waislamu ya kwamba Warumi watawashinda Waajemi karibuni tu, akasema: “ALIF LAM MIYM. WARUMI WAMESHINDWA. KATIKA NCHI ILIYO KARIBU (na nchi ya Arabu, nayo ni Shamu); NAO BAADA YA KUSHINDWA KWAO, WATASHINDA. KATIKA MIAKA MICHACHE; AMRI NI YA ALLAH KABLA (yake) NA BAADA (yake); NA SIKU HIYO WAISLAMU WATAFURAHI. KWA NUSURA YA ALLAH (atakayowapa wao, nayo ni kuwashinda Makureishi siku hiyo). (Allah) HUMUNUSURU AMTAKAYE; NAYE NI MWENYE NGUVU (na) MWENYE REHEMA. (Hii ni) AHADI YA ALLAH, ALLAH HAVUNJI AHADI YAKE, LAKINI WATU WENGI HAWAJUI”. [30:1-6]

 

Na kwa yakini iliwathibitikia waumini ahadi ya Allah, Warumi wakawashinda Waajemi mnamo mwaka 626 A.D. Na wakafanikiwa kuirejesha tena mikononi mwao ardhi yao yote iliyokuwa imekaliwa kimabavu na waajemi. Siku hiyo waumini waliifurahikia nusura ya Allah kwa kuwarudi Makureishi na washirika wao.

 

            ii.          Ulimwengu mzima ulikuwa mithili ya wana-kondoo waliopotea, ukienda katika viza:

 

            Hivi ndivyo ilivyokuwa hali ya kisiasa ya ulimwengu wa Mashariki enzi hizo. Ama hali za kimaadili na kijamii ndizo zilikuwa mbaya mno, tumetaja huko nyuma namna maadili yalivyoporomoka na kufisidika kwa hali za kijamii. Na jinsi dhulma, maasi na uovu vilivyokuwa ndio nembo ya jamii katika kila uma. Na namna gani vurugu lilivyotawala itikadi na kuenea dini za kuabudu masanamu na imani isiyo ya kweli kuzitawala fikra na akili za watu. Na vipi heshima zilivyovunjwa na unyang’anyi, uporaji na uuaji vikawa ndio fakhri ya wenye nguvu. Na ulimwengu wa magharibi haukutofautiana kiufisadi na ulimwengu huu wa mashariki. Jamii ziliporomoka kimaadili mpaka kufikia tabaka ya chini kuliko wanyama na watu kuwa mithili ya kundi la wana-kondoo lililopotea liendalo gizani.

 

Kwa hivyo basi, ilikuwa hapana budi kundi hili la wana-kondoo wapotevu hawa liisikiesauti ya mchungaji ili liweze kuongoza njia. Na ilikuwa lazima lipate kijinga cha moto ili liweze kuongozwa na muangaza wake. Kwa hivyo basi mchungaji akaanza kuliswaga kundi ili lipate kuongoza njia na kuliangazia ili lipate kuona njia. Na mchungaji huyu hakuwa mwingine zaidi ya “Muhammad”; Mtume wa Allah kwa watu wote. Lilikuwa ni jukumu lake baada ya kuisikizisha kaumu yake; Waarabu wenzake sauti yake, ayasikilizishe mataifa yote. Hapo ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoanza kuyaandikia barua za ujumbe wa Uislamu kupitia kwa wafalme wao, ili awatoe gizani kuwatia nuruni.

Additional information