KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

MUAMALA USIO SAWA KWA WATOTO

Sayyidina Abdullah Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-anasimulia kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mtu aliye pata mtoto wa kike na hakumzika akiwa hai, wala hakumdhalilisha na wala hakuwafadhilisha watoto wa kiume juu yake, Allah atamuingiza peponi”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Kwa mujibu wa hadithi hii, kuingia peponi kwa wazazi kunategemea sharti tatu, ambazo ni:

 

1)          Wasiwazike watoto wao wa kike wakiwa hai.

 

2)          Wasiwadhalilishe wala kuwatukana na

 

3)          Wasiwafadhilishe watoto wa kiume juu ya wale wa kike.

 

 

Sharti hili la kwanza; wazazi kuwazika hai watoto wao wa kike, hili kwa sasa halipo kabisa katika Umma wa Kiislamu. Baada ya kudhihiri kwa Uislamu, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kupitia mafundisho yake yagusayo nyoyo na kuziathiri akili. Alifanikiwa kabisa kuitokomeza mila hii ya kishenzi na kikatili na matokeo yake leo hakuna muislamu aishiye juu ya mgongo huu wa ardhi, anaye weza  si kutenda hata kufikiria kutenda jarima hiyo ya kutisha. Lakini bado katika baadhi ya familia jahili za Kiislamu, sharti mbili za mwisho zinapuuzwa. Katika familia kama hizo, watoto wa kiume hupewa kipaumbele kwa wale wa kike, wanapendwa, wanajaliwa na kuthaminiwa zaidi kuliko dada zao.

 

Sababu pekee itolewayo kuhalalisha tabia mbaya hii ya kibaguzi na upendeleo wa wazazi kwa watoto wao wa kiume kwa kuwatweza wale wa kike. Ni ile fikra lemavu kwamba watoto wa kike si wako ni wa watu wengine, wao wanalelewa na kutunzwa kwa ajili ya watu wengine ambao watakuwa mabwana kwao. Wazazi wenye fikra hizo, hawatarajii hata kidogo kwamba wanaweza kusaidiwa au kunufaika kifedha au vinginevyo na watoto wao wa kike. Huwaona watoto wa kike kama mzigo usio na faida kwao tangu kuzaliwa hadi kufa kwao. Wanafikiri kwamba watoto wa kike huzipamba na kuzipa heshima nyumba za watu wengine, wakati ambapo watoto wa kiume ni chanzo na chechem ya matumaini/mategemeo mema kwa nyumba zao wenyewe. Katika familia nyingi, wazazi wana matumaini na matarajio makubwa sana kwa watoto wao wa kiume eti ndio watakao ongeza utajiri na pato la familia. Na ndio nguzo na tegemeo la wazazi uzeeni wakati ambapo watoto wa kike huwagharimu tu pasina faida irudiyo kwa wazazi. Kwa fikra na mawazo potofu haya, watoto wa kiume hufikiriwa kuwa ni rasilimali (Assets) wakati ambapo watoto wa kike huchukuliwa kuwa ni madeni (liabilities) matupu daima. Fikra hizi huwamotisha wazazi kuwalea na kuwatunza watoto wao wa kiume kwa furaha na upendeleo wakati ambapo watoto wa kike hawapewi malezi kama hayo.

 

Kwa kawaida, watoto wa kike katika jamii zetu bado wanaonekana kuwa ni kitu kisicho takikana ambacho kimewalazimu watu. Watoto wa kiume bado wanapendwa zaidi na kuwekwa mbele, wazazi wanajifikiri kuwa ni watu wenye bahati kubwa kwa kuwa na watoto wengi wa kiume. Na  hii ndio sababu, utaona wanashereheka na kufurahikia zaidi uzao wa mtoto wa kiume ukilinganisha na ule wa mtoto wa kike. Hadithi tuliyo inukuu, inaishtumu na kuilaani tabia hii yenye madhara ya wazazi kwa watoto wao. Na inawatahadharisha waislamu kwamba tabia hiyo inamchukiza Allah Mola Muumba wao. Ili kupata radhi zake na kuingia peponi, wazazi wanalazimika kuwatendea watoto wao wa kike na wale wa kiume kwa usawa. Watoto wote; wa kiume na wa kike wapate upendo sawa, matunzo sawa na umuhimu sawa ili wasiugue maradhi ya kisaikolojia. Daima wazazi waongozwe na kanuni na hukumu za Uislamu badala ya kufuata mila zisizo za haki na matashi na matakwa yao binafsi.

 

 

 

       xii.          Mtoto wa kike ni ngao dhidi ya moto:

 

         Kwa mujibu wa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-“Mwanamke mmoja alikuja kwangu kuomba msaada akiwa na watoto wake wawili wa kike. Wakati huo sikuwa na kitu zaidi ya tende moja tu, nikampa tende hiyo pekee, akawagawia mabinti zake na yeye hakula kitu. Kisha akaondoka zake, Mtume wa Allah alipo rudi nyumbani nikamuhadithia mkasa ule. Akasema kwamba mtu yule (mama) aliye jaribiwa kupitia mabinti hawa na ambaye aliwatendea haki. Atawakuta mabinti hao (siku ya Kiyama) kama ngao yake dhidi ya moto wa Jahanam”. [RIYAADHUS-SWAALIHEEN]

Ni kweli kuwa mtoto wa kike anaweza katika baadhi ya hali asiwe chanzo cha manufaa ya kimaada kwa wazazi wake, lakini wanaweza kunufaika nae katika maisha ya akhera kwa msingi wa mwenendo wao mwema kwake. Na hii ndio faida/manufaa maridhawa na manono, kwa sababu kuokoka na moto wa Jahanam ndio matashi na matakwa ya kila muislamu. Kupitia muangaza wa hadithi tuliyo inukuu, wazazi wenye bahati njema ni wale walio ruzukiwa watoto wa kike. Watoto wa kike ambao watakuwa sababu ya wazazi wao wema wenye mapenzi mema kuokoka na moto wa Jahanam. Zaidi ya yote hayo, ni ukweli usio kanushika kwamba watoto wa kike wana mapenzi mno na watiifu zaidi kwa wazazi wao kuliko wale wa kiume.

Additional information