KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

KUNDI LA TATU: WATAWALA NA VIONGOZI

Tambua na ufahamu ewe ndugu mwema-Allah aurudufishe wema wako-kwamba jamii yoyote ya wanadamu haina budi kuwa na watawala/viongozi. Hilo ni suala wasilo jikwasia nalo, hawana njia/namna ya kuliepuka. Na uongozi/utawala ni suala nyeti mno na viongozi wako katika nafasi ngumu na kwenye dhima nzito. Kwani wao wakitekeleza haki ya Allah inayo walazimu katika huo uongozi na haki za waja wake, huchoka na kukimwa. Na wakizipoteza haki hizo, huhiliki na kuangamia. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: "Nyote nyinyi ni wachunga na nyote nyinyi mtawajibika kwa uchunga wenu". Na akasema tena: "Hakika nyinyi mtauwania uongozi na hakika huo (uongozi) utakuwa majuto siku ya Kiyama". Mahala pengine akasema: "Ewe Mola wa haki! Atakaye tawalia chochote katika suala la umati wangu, akawadhiki basi nawe mtie dhiki. Na atakaye tawalia chochote katika suala la umati wangu, akawaonea huruma basi nae muhurumie". Akasema tena: "Hapana kiongozi yeyote wa watu ila ataletwa siku ya Kiyama ikiwa imetiwa pingu mikono yake shingoni kwake. Uadilifu wake ndio utakao mfungua au dhulma yake ndio itakayo mdidimiza".

 

Na makamio yaliyo pokewa katika upande wa mtu aliye tawalia mambo ya watu, halafu asifuate uadilifu na insafu na kujiepusha na dhulma, ni makali mno yenye kutisha. Ni kwa ajili hii basi, ndio wacha-Mngu wakaupa nyongo uongozi na wakaukimbia wapanyao ambao wao hao kwa ajili ya kumuogopa Bwana Mlezi wao wananyenyekea. Na atakaye onjwa miongoni mwao kwa kupewa uongozi na akawa hana budi, basi katika upeo wa khofu na unyenyekevu na kujihifadhi na kujikinga. Hata Umar Ibn Khatwaab-Allah amuwiye radhi-pamoja na ukamilifu wa uadilifu aliokuwa nao na upeo wa kujichunga, alifikia kusema: "Nani atakaye utwaa (uongozi) kwa yaliyomo humo, ningelipendelea kwamba mimi niokoke humo nikiwa nimetoshewa. Sina dhima juu yangu wala haki yangu". Na likuwa kutoka na na hofu yake kuu ya kupoteza chochote katika mambo ya waislamu na umakini wake katika hayo, halali ila kwa mang'amung'amu na akikaa na kusema: "Nikilala mchana ntapoteza mambo ya waislamu na nikilala usiku nitaipoteza nafsi yangu, basi nitalalaje baina ya viwili hivi?".

 

Na alikuwa Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-inapo kusanywa mali katika Baytul-Maal (Hazina) ya waislamu, huwaita na kuwagawia hata isibakie humo walau Dirham moja. Kisha huamrisha ifagiliwe na kupigwa deki na huswali humo na kusema: "Kama itakavyo shuhudia juu yangu kwa kukusanya mali ndani yake, inishuhudie kwa kuswali ndani yake (pia)".

 

Na zama Umar Ibn Abdil-Aziyz-Allah amuwiye radhi-alipo tawalia ukhalifa-kikasikiwa nyumbani kwake kilio kikubwa sana. Watu wakauliza sababu yake, pakasemwa: Hakika yeye amewakhiyarisha wake zake na masuria baina ya kutowaendea au kuwataliki na akasema: "Hakika mimi nimeshughulishwa kiasi cha kutoweza kuwa nanyi kwa sababu ya majukumu ya uongozi wa waislamu nilio kalifishwa". Basi wao wakakhitari kukaa pamoja nae katika hali hiyo. Imepokewa kwamba yeye hakupata kuoga kutokana na janaba katika muda wote wa ukhalifa wake ila mara mbili tu. Na kipindi cha ukhalifa wake kilikuwa karibu miaka miwili na nusu. Siku moja alitaka kuoga, akaletewa maji ya moto ndani ya ndoo ya shaba na kulikuwa na baridi kali. Akauliza: Mmeyachemshia nini maji haya? Akajibiwa: Kwenye jiko la uma. Akakataa kuyaoga maji hayo na badala yake akataka kuoga maji baridi, khadimu (mtumishi) akamwambia: Ukiyaoga maji baridi haya, watu watapambazukiwa wakiwa hawana khalifa (yaani utakufa kutokana na baridi kali). Akasema: Nitafanyaje na ilhali maji haya (ya moto) si halali kwangu? Khadimu akamwambia: Thamini kuni ambazo zinachemsha maji kama haya na uitie thamani hiyo katika Baytul-Maal ya waislamu. Basi nae akaithamini na kuirudisha katika Baytul-Maal.

 

Na sira za makhalifa waongofu-Allah awawiye radhi-katika mfano wa haya ni maarufu zenye kutangaa, kunarepa kuzitaja kwake. Lakini hilo halikutimia kwa wajihi wake kama itakikanavyo ila kwa makhalifa wanne; Abu Bakri, Umar, Uthman na Aliy-Allah awawiye radhi. Na ulikuwa muda wa ukhalifa wao ndio ule alioutaja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: "Hakika jambo (dini) hili limeanza kwa utume na rehema, halafu utafuatia ukhalifa na rehema, kisha utakuwa ni ufalme na nguvu...". Na akasema: "Ukhalifa baada yangu ni miaka thelathini". Basi ukawa muda huu ndio kipindi cha makhalifa wanne kwa kuongezea na siku ambazo  alishika ukhalifa ndani yake Al-Hasan Ibn Aliy; mjukuu wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nazo ni kiasi cha miezi sita. Ikatimia kwa muda huo miaka thelathini tangu kufariki kwa Mtume wa Allah mpaka pale Al-Hasan Ibn Aliy-Allah awawiye radhi-alipofanya suluhu na Muawiyah Ibn Abi Sufyaan. Na akambai pale alipoyaona alioyaona na kutambua aliyoyatambua. Na yakatimia kwake yale aliyoahidiwa na babu yake; Mtume wa Allah, pale aliposema: "Hakika mwanangu huyu ni Bwana na huenda Allah akasuluhisha kupitia kwake baina ya makundi mawili ya waislamu". Hayajapata kuwepo katika zama za Uislamu tangu alipokufa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mpaka leo hii. Siku wala zama ambazo kuna ndani yake uadilifu, ihsani na kuondoshwa dhulma na uadui na kusimamishwa haki na dini, na kupigana jihadi na makafiri. Muda/kipindi kinacho fanana wala kukaribiana na kipindi cha ukhalifa wa makhalifa waongofu. Ambacho ndio ile miaka thelathini iliyotajwa katika kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

 

Naam, bila ya shaka amepita/ameshika mfano wa mwendo wao na karibu sana, khalifa mwema; Umar Ibn Abdil-Aziyz Al-Amawiy-Allah amrehemu. Lakini ulikuwa mfupi muda wa ukhalifa wake na alikumbana na taabu na mashaka makubwa kutoka kwa watu wake, khususan watu wa nyumbani kwake. Hiyo ni kwa sababu zilisha wambalikia watu zama za uadilifu na usimamishaji wa haki. Na hilo ni tangu pale Al-Hasan Ibn Aliy alipombai Muawiyah-Allah awawiye radhi-mpaka pale alipotawazwa khalifa Umar Ibn Abdil-Aziyz. Na hilo ni kiasi cha miaka sitini, zikafutika ndani ya kipindi hiki nyingi ya suna/taratibu za uadilifu na insafu. Na zikadhihiri humo nembo za dhulma na watu wakakengeuka na njia ya sawa, hilo likamuwia ugumu Umar Ibn Abdil-Aziyz kuwarudisha katika hali kama aliyo kuwa nayo yeye. Mpaka imetufikilia khabari kwamba Umar Ibn Abdil-Aziyz alimuomba mmoja wa waja wema wa Allah amuombee kushukiwa na mauti. Pale alipozidiwa mno na uongozi wa watu, na kumuwia ugumu kutekeleza haki na uadilifu kama itakikanavyo. Kwa sababu hiyo, akakhitari mauti na kwenda kwenye nyumba ya akhera ambayo hiyo ni bora na yenye kusalikia milele. Na wala hili kwake halikuwa kwa sababu ya kupapatika na kukimwa, la hasha. Lakini ni kwa ajili ya kuchelea kukabiliwa na wachukivu wa dini ya Allah, na kusimamisha uadilifu katika waja wake. Miongoni mwa wapendao dhulma na kula mali za watu kwa batili, wasije kumkabili kwa jambo asilo liweza. Na kupelekea fitina, ikhtilafu na mtengano baina ya waislamu, ni kwa ajili hii ndio akayakhitari yaliyoko mbele ya Allah.

Naye alikwisha tanguliwa katika hili na Amirul-Muuminina; Aliy Ibn Abiy Twaalib-Allah amuwiye radhi. Pale watu wa Iraq walipo khitilafiana nae na akaona kwao ajizi na ngojangoja katika kuinusuru haki na kupambana na madhalimu. Mpaka imepokewa kwamba yeye alisema: "Ewe Mola wa haki! Nipumzishe nao na uwapumzishe nami". Akamuona Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-usingizini, akamshitakia ikhtilafu na mizozo aliyoipata kutoka kwa umma, Mtume akamwambia: "Muombe Allah dhidi yao". Aliy akaomba: "Ewe Mola wa haki! Nibadilishie watu bora kuliko wao na wao uwabadilishie (kiongozi) muovu kuliko mimi"

Additional information