KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

DONDOO ZA WIKI

JAMVI LA RAMADHANI : “TUIKARIBISHE NA TUIPOKEE RAMADHANI KWA TWAA NA SI KWA MAASIA KAMA ILIVYO ZOWELEKA NA WASIO IJUA THAMANI YA RAMADHANI”

Sifa zote njema ni zake Allah aliye ukirimu ummati Muhammad kwa neema ya mwezi wa Ramadhani, neema ambayo hazikupewa umma zilizo tangulia. Na Rehema na Amani zimuendee Mtume aliye letwa kwetu kutubainishia halali na haramu na kuwaonya waendao kinyume na maamrisho ya Mola Muumba wao kufikwa na adhabu kali. Na kuwapa bishara njema ya kupata neema ya milele wale wote watakao ishi kwa kufuata muongozo wa Mola wao. Rehema na Amani pia ziwashukie Aali na swahaba zake wote na jamia waumini mpaka siku ya Kiyama.

Ama baadu,

Mpendwa ndugu yetu katika Imani.

Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Ni jambo jema, tena la wajibu, tuanze kwa kumshukuru Mola wetu Muweza wa kila kitu ambaye kwa uwezo na matashi yake, ametujaalia uhai na uzima hata tukaweza kukutana kwa mara nyingine tena katika ukumbi wetu huu wa Ramadhani. Mola wetu Mtukufu tunakuomba utuzawadie ufahamu utokao kwako ili tuweze kuiona Ramadhani kuwa ni neema, zawadi na fursa ghali ya utakaso, muono ambao utakuwa ni kani ya kutusukuma kuitumia vema fursa hii kutenda amali njema zitakazo tuzawadia mavuno tunu ndani ya mwezi huu. Matendo ambayo yataifanya Ramadhani itushuhudilie kwa wema pale tutakapo simama mbele yako katika siku ile ya hukumu adilifu na jazaa sawiya.

Ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-tukiri na tukubali ya kwamba hakuna kiumbe anaye ijua fika thamani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kumshinda Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na wala hakuna kiumbe aliye ifunga vilivyo swaumu ya Ramadhani kumshinda Mtume wa Allah kama ambavyo hakuna kiumbe aliye nufaika na Ramadhani kuliko Mtume wa Allah. Na kwa kuwa Mola Muumba wetu anatuambia:

Hakika nyinyi mnayo ruwaza (kigezo) njema kwa Mtume wa Allah, kwa anaye mtaraji Allah na siku ya mwisho, na akamkumbuka Allah sana”. Al-Ahzaab [33]:21

Read more...

VYAKULA NA VINYWAJI WAKATI WA DHARURA

Huvuliwa/hutolewa kutoka katika uenevu wa hukumu ambayo imeizaa misingi mitatu hii tuliyo itaja, hali ya dharura iliyo mkwaza mtu. Ni halali kwake atakapo songeka kula nyamafu aliye harimishwa na hayawani ambao umethibiti uharamu wa kuwala. Ale kiasi cha kumtia nguvu na kumbakishia uhai wake, na hivyo ni kwa kuitia vitendoni kauli yake Allah Atukukiaye: “...WALA MSIJIUE. HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUWAREHEMUNI”. [4:29] Na kauli yake: “...NA MWENYE KUSHURUTISHWA NA NJAA, BILA YA KUPENDELEA DHAMBI, BASI HAKIKA ALLAH NI MSAMEHEVU NA MWENYE KUREHEMU”. [5:03] Na kauli yake: “...LAKINI ALIYE FIKIWA NA DHARURA BILA YA KUTAMANI WALA KUPITA KIASI, YEYE HANA DHAMBI. HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUSAMEHE, MWENYE KUREHEMU”. [2:173]

Endelea

UTEKELEZAJI WA AHADI ...Inaendelea/4

Kutekeleza haki ni WAJIBU bila ya kumuangalia huyo mstahiki wa kutekelezewa ni muislamu au sio muislamu. Kwa sababu kwamba jambo hilo tukufu/jema haligawiki hata ikawa mtu awe duni/dhalili akiwa pamoja na watu fulani na awe mtukufu/muheshimiwa akiwa pamoja na watu fulani. Muhimili wa mahala pa ahadi, muda wa kuwa ahadi hiyo ni kheri/wema, kuikiri kwake ni wajibu unao pasa kutekelezwa kwa kila mtu na kila wakati. Hili Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikwisha lisema katika kiapo cha fudhuli, hiki ni kiapo kilicho fanywa katika jahiliya: “...lau nitalinganiwa kwayo hiyo (ahadi) katika Uislamu, ningeli itika...”.

Endelea

KHABARI ZA AL ASWAD

Waislamu walipo ifungua nchi ya Yemen na kuwa chini ya himaya ya mamlaka ya Kiislamu, katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Mtume akamtawadha Baadhaan Al-Faarisiy kuwa gavana wa Yemen, huyu ni Mfursi wa Iran ambaye alipelekwa Yemen na Kisraa (mfalme) Abrawiyz kuwa gavana huko kwa niaba yake. Akaendelea kumuwakilisha Kisraa huko mpaka Mtume wa Allah alipo twaa madaraka ya huko, nae ndiye aliye funga ukurasa wa magavana wa Kifursi walio itawala Yemen. Baada ya utawala wa Yemen kuangukia mikononi mwa waislamu, Baadhaan akasilimu na ndipo Mtume akambakisha katika wadhifa wake wa ugavana. Na makao yake makuu yalikuwa katika mji wa Sanaa.

Endelea

MAZUNGUMZO BAINA YA MUUMBA MTUKUKUA NA BAADHI YA WAJA WAKE...Inaendelea/3

Na yanayo kujia sasa ni mazungumzo jibizani mengine yaliyo jiri baina ya Ibrahimu-Amani imshukie-na Muumba wake-utakati wa mawi ni wake. Nayo yanafahamisha juu ya ukamilifu wa uweza wa Allah Ataadhamiaye na mahaba ya Ibrahim kutaka kufika lindini mwa daraja za imani. Qur-ani Tukufu imetusimulia mazungumzo hayo kupitia kauli yake Allah Atukukiaye: “NA ALIPO SEMA IBRAHIM: MOLA WANGU MLEZI! NIONYESHE VIPI UNAVYO FUFUA WAFU. ALLAH AKASEMA: KWANI HUAMINI? AKASEMA: HASHA! LAKINI ILI MOYO WANGU UTUE. AKAMWAMBIA: TWAA NDEGE WANE NA UWAZOESHE KWAKO, KISHA UWEKE JUU YA KILA KILIMA SEHEMU, KISHA WETE, WATAKUJIA MBIO. NA UJUE KWAMBA HAKIKA ALLAH NI MTUKUFU MWENYE NGUVU, NA MWENYE HIKIMA”. [02:260]

Endelea

Additional information