Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Fiqh na Sheria  

"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

WASIA WA UANGALIZI


SOMO LA NNE


WASIA WA UANGALIZI.


  1. Fasiri ya wasia wa uangalizi:

Wasia wa ungalizi/usimamizi ni tafsiri ya neno la Kiarabu “Iiswaau”, neno ambalo limeteuliwa na Mafaqihi (Wataalamu wa fani ya Fiq-hi) kuwakilisha/kuelezea dhana nzima ya mtu: Kumuusia mtu aliye na imani naye, kabla ya kufa kwake, kuwaangalia/kuwasimamia watoto wake, kuteleza wasia wake, kulipa madeni yake, kurejesha amana za watu zilizoko kwake na mfano wa hayo, baada ya kufa kwake.

  1. Fasiri ya wasii (msimamizi wa mali/haki/wasia):

Kutokana na maelezo yaliyo tangulia, inabainika maana ya wasii, ya kwamba yeye ni yule mtu ambaye anaye pewa majukumu ya kusimamia masuala ya watoto (wa marehemu). Kurejesha amana na kulipa madeni kwa niaba ya marehemu.


  1. Hukumu ya wasia wa uangalizi:

Lililo asili katika wasia wa uangalizi, ni kwamba huo umesuniwa, lakini unaweza kuingiwa na mambo yatakayo ufanya kuwa wajibu.

Imamu Al-Adhra’iy-Allah amrehemu-amesema: “Inadhihiri ya kwamba ni wajibu kwa akina baba kuusia katika masuala ya watoto, pale itakapo kuwa hawana babu mstahiki wa utawala. Kumpa wasia huo mtu muaminifu, mwenye kuheshimika, atakapo mpata. Na akawa na dhana yenye nguvu ya kwamba yeye akiacha wasia, mali yake itatawaliwa na mtu mwenye khiana, yaani kadhi au mwenginewe katika watu madhaalimu. Kwani kumemuwajibikia kuihifadhi mali ya watoto wake, isipotee”.

Na amesema Imamu Al-Baajuuriy-Allah amrehemu: “Wasia wa uangalizi ulio tajwa ni Sunna, ila katika kukidhi (kulipa) haki aliyo shindwa (kuikidhi) hivi sasa (katika uhai wake) na ambayo haina mashahidi. Basi hakika wakati huo wasia wa uangalizi unakuwa ni wajibu, kwa sababu kuacha kuusia kunapelekea kupotea kwa haki hiyo”.

Kutokana na maelezo yaliyo tangulia, inabainika ya kwamba kuusia uangalizi/usimamizi ni wajibu pale itakapo kuwa mwenye kuusia anazo haki zake kwa watu (anadai) au watu wanazo haki zao kwake (anadaiwa). Ambazo dhana yake kubwa ni kwamba haki hizo zitapotea kama hakuusia suala la kuzifichua na kuiweka wazi kadhia yake kwa mtu atakaye chukua mahala pake.

Na hali kadhaalika itakapo chelewa (ogopewa) watoto wadogo kupotea au kupata madhara, hakika ni wajibu kwa baba yao kutoa wasia kwa mtu anaye muamini, ili apate kuangalia/kusimamia mambo yao na achunge maslahi yao.

Ama iwapo hakuna lolote katika hayo yaliyo tajwa, hakika kuusia uangalizi/usimamizi linabakia kuwa ni suala la Sunna na kitendo chenye kupendelewa na Sharia.


  1. Hekima/Falsafa ya kuwekwa kwa Sharia ya wasia wa uangalizi/usimamiaji:

Hekima/falsafa ya kufanya wasia wa uangalizi/usimamizi kuwa ni jambo la kisharia, ni ule uhitajiwa wake na jamii na kutekelezeka kwa maslahi ya watu kupitia wasia huo.

Inawezekana mtu akawa katika hali ya kuchungulia kaburi (karibu ya kufa) na yakawa yapo baina yake na jamii inayo mzunguka, mahusiano ya kimaada. Kama vile amana zake zilizoko kwa watu au viazimwa vyake vilivyoko kwao au viazimwa vyao vilivyoko kwake. Na wakati mwingine huenda akawa na madeni yanayo muwia, akahitajia mtu atakaye simamia ulipaji wa madeni hayo kwa niaba yake, baada ya kufa kwake. Na inaweza kutokezea akawa na watoto wasio jiweza, hawana uwezo wa kuendesha shughuli za mali iliyo achwa na marehemu mzee wao. Kwa ajili/sababu hiyo basi, maslahi ya watoto hao yakahukumia/yakapelekea kuwekwa mtu mwenye ujuzi katika shughuli hizo, ili apate kuyasimamia yote hayo. Ni kwa sababu ya kuyaangalia/kuyazingatia yote hayo, ndipo Uislamu ukaufanya wasia wa uangalizi/usimamizi, kuwa ni jambo la kisharia na ukalihimiza na kuliraghibisha (kulipendezeshea nyoyo).


  1. Shartia za Wasia:

Tumesha sema kwamba wasii ni yule mtu anaye pewa majukumu ya uangalizi/usimamizi baada ya kufariki Dunia kwa mwenye kuusia (muweka msimamizi). Na ili huyu wasii aweze kuyatekeleza majukumu aliyo pewa kwa namna bora kabisa, hapana budi zipatikane kwake sharti zifuatazo:

    1. Awe ni mtu mkalafu; yaani awe baleghe (aliye fikia umri wa utu-uzima) na mwenye akili timamu. Kwani asiye baleghe, mwenye akili timamu anastahiki kupata wa kutawalia mambo yake na kuyasimamia masuala yake, basi inawezekanaje kukaswihi kumpa utawala, ili atawalie mambo ya mwingine?!

    2. Awe muungwana (mtu huru), kwa kuwa mtumwa hana usarifu katika mali ya baba yake. Kwa ajili/sababu hiyo basi, hafai kuwa wasii anaye sarifu (panga/dhibiti utumizi, au ustawishaji) katika mali ya mtu mwingine hata kama atapewa idhini na bwana mmiliki wake.

    3. Awe muislamu na sharti hili ni katika utawalia wa muislamu. Kwa muktadha wa sharti hili basi, hakuswihi kumpa kafiri wasia wa uangalizi/usimamizi, ili ayatawalie mambo ya Waislamu, kwani yeye ni mtuhumiwa, na Allah hakumpa utawala juu yao (hao Waislamu). Allah Ataadhamiaye anasema: “...WALA ALLAH HATAWAPA MAKAFIRI NJIA YA KUWASHINDA WAUMINI”. [04:141]

Na amesema-utakati wa mawi ni wake: “ENYI MLIO AMINI! MSIWAFANYE WASIRI WENU WATU WASIO KUWA KATIKA NYINYI, HAWATAACHA KUKUFANYIENI UBAYA...” [03:118]

Wasiri wenu: Marafiki wanao ingia katika mambo yenu na mkawa mkiwapa siri zenu. Hao hawataacha kuyafisidi mambo yenu.

Lakini unaswihi wasia wa uangalizi/usimamizi wa dhimiyu kwa dhimiyu na kadhaalika dhimiyu kwa muislamu.

    1. Awe muadilifu, asiye jizamisha katika madhambi makubwa wala kuendelea kuyashikilia madhambi madogo. Na unatosha kwake uadilifu wa nje; yaani dhaahiri ya hali yake iwe hivyo. Kwa uzingatiaji wa sharti hili basi, hakuswihi kumuusia uangalizi/usimamizi mtu fasiki, kwa kuwa wasia ni utawala na uaminiwa, na mtu fasiki sio muaminiwa.

    2. Awe ni mstahiki wa usarifu (upangaji/udhibiti wa utumizi/ustawishaji) wa kilicho usiwa (kusimamiwa/kuangaliwa) na awe na uwezo juu ya hilo. Kwa mujibu wa sharti hili basi, hakuswihi kumpa wasia wa usimamizi/uangalizi mtu safihi, mgonjwa, mkongwe, mwenye matatizo ya akili na aliye msahaulifu. Kwa kuwa hakuna maslahi kumpa utawala mtu ambaye hali yake ndio hiyo.

Hivi ndivyo ilivyo, na kutokana na sharti za wasii zilizo tajwa, inapatikana faida ya kwamba kunajuzu kumpa wasia wa uangalizi/usimamizi:

      1. Kipofu, kwa kuwa anaweza kuwakilisha katika masuala ambayo hawezi kuyajua yeye mwenyewe.

      2. Mwanamke, kwani yeye anafaa kwa kazi ya usarifu.

Sayyidna Umar bin Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-wakati wa kufa kwake alimpa wasia wa uangalizi/usimamizi binti yake Hafsah-Allah amuwiye radhi.

Abu Daawoud [2789]-Allah amrehemu.

Bali yeye huyo mwanamke ndiye aula (bora zaidi) kuliko wenginewe katika kupewa wasia wa uangalizi/usimamizi, pale zitakapo kusanyika kwake sharti za wasii, kwa sababu ya huruma yake nyingi aliyo nayo kwa watoto wake kuliko yeyote asiye yeye.


  1. Hukumu zinazo fungamana na wasii na wasia wa uangalizi/usimamizi:

Kuna mjumuiko wa hukumu nyingi zinazo fungamana na wasii na wasia wa uangalizi/usimamizi, tunazitaja kwa ufupi kama ifuatavyo:

    1. Hakumuelei (hakumjuzii) wasii kumpa mtu mwingine wasia huo wa uangalizi/usimamizi. Kwa sababu mwenye kuusia (muweka msimamizi) alimchagua yeye na hakuuridhia usarifu wa mtu mwingine. Hayo ni iwapo mwenye kuusia aliuacha huru wasia, bila ya kuufunga na sharti au alieleza wazi kutokuwakilisha. Ama atakapo mpa idhini ya kufanya hivyo, basi hakika yeye hazuiwi kufanya hivyo.

    2. Kunajuzu katika wasia wa uangalizi/usimamizi kuweka muda na kufungamanisha na kitu/jambo.

Lau muweka wasia atasema: “Nimempa fulani wasia wa uangalizi/usimamizi mpaka atakapo baleghe mwanangu”, au “mpaka atakapo kuja kaka yangu”, hilo linajuzu. Na kadhaalika lau atasema: “Nitakapo kufa, basi nimesha kupa wasia wa uangalizi/usimamizi”, hakika hilo linajuzu, kwa sababu kuusia uangalizi/usimamizi kunachukua uwezekano wa umajuhuli na fikra za moyo. Na kwa sababu wasia wa uangalizi/usimamizi ni kama kutawaza uongozi. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimpa uongozi wa jeshi Zaid bin Haaritha-Allah amuwiye radhi-katika vita vya Mu’utah na akasema: Akiuawa Zaid, uongozi ushikwe na Ja’afar na akiuawa Ja’afar, basi uongozi ni wa Abdullah bin Rawaahah. Bukhaariy [4013]-Allah amrehemu.

    1. Lau mtu atatoa wasia wa uangalizi/usimamizi kwa watu wawili na asimpe yeyote kati yao uwezo wa usarifu peke yake bila ya mwenzake, bali alishurutiza kukusanyika wote wawili katika huo (usarifu), au aliuacha huru, akasema: “Nimemuusia Zaid na Amrou”. Mmoja wao hawezi kupwekeka na usarifu peke yake, hivyo ni kwa kuifanyia kazi ile sharti ya kwanza na kutokana na shaka katika ile sharti ya pili.

Lakini lau mwenye kuusia (muweka msimamizi) atafumbuliza wakati wa kuusia kila mmoja wao kuwa peke yake katika usarifu, kama vile kusema: “Nimemuusia kila mmoja kati yenu”, au “kila mmoja kati yenu ni wasii”. Kumemjuzia kila mmoja kati yao kusarifu peke yake, bila ya kuwa na mwenzake, kwa sababu ya kuwepo kwa idhini ya hilo kutoka kwa mwenye kuusia.

    1. Kifungo (mkataba) cha wasia wa usimamizi/uangalizi, ni kifungo jaaizi (chenye khiyari) kwa pande zote mbili. Kwa hivyo basi, kunamuelea wasii (msimamizi/muangalizi) kujiuzulu yeye mwenyewe (katika uangalizi/usimamizi) wakati wowote anapo taka, kama ulivyo uwakala, kwani yeye ni muwakilishi wa mwenye kuusia. Lakini kujiuzulu huko kutaswihi iwapo kama haikuwa wajibu juu yake kuusimamia/kuutekeleza wasia. Na haikuelekea kwenye dhana yake kutilifu mali ya mwenye kuusia kwa kutawaliwa mali yao na dhaalimu miongoni mwa kadhi na mwenginewe. Akichelea lolote katika hayo, hakumjuzii kujiuzulu yeye mwenyewe na wala kujiuzulu kwake hakutapita, kwa ajili ya kuchunga maslahi ya mayatima na kuwaondoshea wao hatari au mali yao.

    2. Kunashurutizwa katika kuusia masuala ya uangalizi wa watoto, awe huyo mwenye kuusia ni miongoni mwa wale walio na utawala juu yao, kama vile baba au babu.

Wala hakumjuzii baba kumuweka mtu kuwa wasii juu ya watoto wake na ilhali babu yao yu hai na anazo sifa za utawala. Kwa kuwa utawalia wake umethibiti kisharia, basi hakumuelei kuuhamisha utawaka kutoka kwake, kama ulivyo utawalia wa kuozesha.

    1. Mtoto wa mwenye kuusia atakapo baleghe na akazozana na wasii katika utumizi wa mali na akadai ya kwamba yeye anafanya ubadhirifu. Katika hali/mazingira hayo, wasii atasadikiwa kwa yamini yake, kwa kuwa yeye ni muaminiwa mbele ya sharia.

Lau atazozana nae katika kuikabidhi mali kwake baada ya kubaleghe, katika hali/mazingira hayo atasadikiwa mtoto kwa yamini yake, na hili ni kwa mujibu wa eleweko (mafuhumu) ya kauli yake Allah Ataadhamiaye: “...NA MTAKAPO WAPA MALI YAO WASHUHUDIZIENI...” [04:06] Yaani: Na mnapo wakabidhi mayatima mali yao, wekeni mashahidi wa kushuhudia hilo.



   



| Tuandikie |