|
Hakika urafiki ni wajibu utegemee na ujengeke juu ya nguvu za imani
na matendo matukufu. Na bora ya wanacho kidaimisha watu ni tangamano
lao na yatasalia duniani na akhera mawada (mapenzi dhati) yao, wale
walio kusudiwa na hadithi: “Atakaye amiliana na watu,
asiwadhulumu, akazungumza nao asiwaongopee, na akawaahidi na
asiwakhalifie miadi yake. Basi huyu ni katika wale ambao umekamilika
murua wao na umedhihiri uadilifu wao na umepasa udugu wao”.
Mahusiano ya kirafiki yatakapo anzishwa kwa ajili ya Allah, basi
hayatasalia na kumea ila kwa kumtii Yeye Allah. Na wala hayatakuwa na
kuendelea ila kwa marafiki wawili hao kujiepusha na unafiki na
ufisadi. Angalia, maasi yatakapo penya na kuingia kwenye silka na
mwenendo wa aidha mmoja wao au wote wawili, hapo nyoyo hubadilika na
mapenzi hukauka. Imekuja katika hadithi: “Naapa kwa yule ambaye
nafsi yangu iko mkononi mwake, hawakupendana wawili kisha
wakafarikiana, ila ni kwa sababu ya dhambi anayo itenda mmoja wao”.
Ibn Abi Dunya-Allah amrehemu.
Ni kwa ajili hiyo basi, ndio maswahaba wa Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-wakawa wanakufanya kuhusiana haki na kusaidiana
katika kutenda kheri/wema. Mawili hayo ndio uzio/wigo unao yahifadhi
mawada (mapenzi dhati) yaliyo baina yao, na unawakurubishia kwenye
msamaha na radhi za Allah. Imepokewa kutoka kwa Abu Qalaabah,
amesema: “Watu wawili walikutana sokoni, mmoja wao akamwambia
mwenzake: Njoo tumuombe maghufira Allah katika mahala pa mghafala wa
watu, wakafanya hivyo. Mmoja wao akafa, mwenzake akakutana naye
usingizini, akasema: Nimejua ya kwamba Allah ametusamehe madhambi
yetu jioni ya siku ile tuliyo kutana sokoni”.
Na imepokewa kutoka kwa Anas bin Maalik-Allah amuwiye radhi: Alikuwa
Abdullah bin Rawaahah anapo kutana na mtu katika maswahaba wa Mtume
wa Allah, husema: Njoo tumuamini (tumdhukuru) Mola wetu kitambo
kidogo. Siku moja akamwambia maneno hayo mtu mmoja, mtu yule
akaghadhibika. Akaenda kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akasema: Ewe Mtume wa Allah! Kwani humuoni mwana wa
Rawaahah, anaichukia (anatoka) imani yako na kwenda kwenye imani ya
kitambo kidogo? Mtume akasema: “Allah amrehemu mwana wa Rawaahah,
hakika anavipenda vikaazi ambavyo malaika hujifakharisha navyo”.
Ahmad & Twabaraaniy-Allah awarehemu.
Na inatakikana marafiki wajuane na kufahamiana ili kuhusiana kwao
kuwe juu ya ushahidi na mmoja wao amwambie mwenzake mapenzi na uenzi
alio nao juu yake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Mmoja wenu atakapo mpenda nduguye (muislamu mwenzake), basi na
amwambie ya kwamba yeye anampenda”. Ahmad-Allah amrehemu.
Na imepokewa kutoka kwa Anas-Allah amuwiye radhi: Mtu mmoja
alikuwa kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akapita mfu
fulani. Akasema: (yule aliyeko kwa Mtume): Hakika mimi ninampenda
huyo (apitaye). (Mtume) akasema: Je, umemjulisha? Akajibu: Hapana.
(Mtume) akasema: Basi mjulishe. Akamuendea na kumwambia: Hakika mimi
ninakupenda kwa ajili ya Allah. Akasema (mtu mpendwa yule): Akupende
Allah ambaye kwa ajili yake wewe umenipenda mimi”. Abu
Daawoud-Allah amrehemu.
Na amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Mtu
atakapo funga udugu na mtu, basi na amuulize (huyo nduguye) jina
lake, ubini wake (jina la baba yake) na ukoo wake, kwani hilo
hupelekea zaidi kwenye mawada”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.
Na wala hapana shaka kwamba ufanyaji wa mzaha (utani halali/kweli) na
ufikiri wa mambo, una mlango mkubwa katika uasisi wa mahusiano ya
urafiki, pamesemwa: “Huenda akawa nduguyo wa dhati/ukweli, yule
ambaye hamkuzaliwa na mama mmoja”. Kwani huenda ikatokezea
katika mchakato wa maisha, mtu akakutana na ambaye anahisi kuoana
naye kitabia na kuvutika naye mno, kama kwamba wamejuana miaka mingi.
Na hayo ni usadikisho wa hadithi: “Roho ni majeshi yaliyo
tayari, zilizo fahamiana katika hayo (majeshi) huungana pamoja na
kuzoeana na zilizo kataana katika hayo hutofautiana”.
Bukhaariy-Allah amrehemu.
Lakini hisia hizo ni wajibu zitawaliwe na mamlaka ya imani na nidhamu
yake. Madaraka hayo ambayo muumini huwa nayo katika mielekeo yote ya
moyo wake, ndio humfanya kumpenda kwa ajili ya Allah yule ambaye
hajapata kumuona ana kwa ana, kwa sababu ya umbali wa masafa baina
yao au kuishi katika zama mbili tofauti. Na kwa ajili hiyo hiyo,
kadhaalika humchukia yule ambaye hajapata kuchanganyika pamoja naye
si katika mji au safarini. Yote hayo si kwa ajili ya chochote ila tu
ni kwamba yeye anawapenda wema na anawachukia waovu. Na mielekeo ya
moyo kwa namna hii takasifu, humnyanyua mdau wake daraja nyingi juu
ya cheo chake stahiki. Imepokewa kutoka kwa Abu Dharri-Allah amuwiye
radhi: Nilisema: Ewe Mtume wa Allah! Mtu anawapenda watu lakini
yeye hawezi kufanya amali wanazo zifanya watu hao. (Mtume) akasema:
“Wewe Abu Dharri utakuwa pamoja na uwapendao”. Tirmidhiy-Allah
amrehemu.
Na miongoni mwa taratibu za Uislamu katika suala zima la mahusiano ya
kirafiki, ni kutembeleana ambako hakubebi lengo lingine lolote zaidi
ya kukusudia kupata radhi za Allah kupitia mlango huo wa kupenda kwa
ajili yake. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye
radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Ya
kwamba mtu mmoja alimtembelea ndugu yake (wa imani) katika kitongoji
fulani. Allah akamletea malaika akiwa njiani (kuelekea huko), alipo
mfikia akamuuliza: Unakwenda wapi? Akajibu: Ninakusudia kumzuru ndugu
yangu katika kitongoji hiki. (Malaika) akauliza (tena): Je, kuna
neema unayo ikusudia (kuipata kutoka kwake)? Akajibu: Hapana, ila tu
ni kwamba mimi nimempenda kwa ajili ya Allah Ataadhamiaye. Akasema
(yule malaika): Basi hakika mimi ni mjumbe wa Allah kwako, (nimetumwa
nikubainishie) ya kwamba Allah amesha kupenda kama ulivyo mpenda kwa
ajili yake”. Bukhaariy-Allah amrehemu.
Hakika hatua hizi anazo piga mtu kwenda kumtembelea ndugu yake wa
imani, ni ghali mno. Hakika hatua hizo, ni kama zile hatua za
mujahidina katika njia ya Allah, zinazo jizolea thawabu maridhawa
mno. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakaye
mkagua mgonjwa au akamtembelea ndugu yake katika Allah, atalinganiwa
na mlinganiaji: Umetenda vema na yamekuwa mema matembezi yako na
umesha jipotelea nyumba peponi”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.
Na amesema: “Hapana mja yeyote anaye enda kumzuru nduguye kwa
ajili ya Allah, ila hulinganiwa na mlinganiaji kutoka mbinguni ya
kwamba umetenda vema na pepo imekuwa njema kwako. Na zaidi ya hivyo,
Allah atasema katika ufalme wa Arshi yake: Mja wangu amefanya ziara
kwa ajili yangu na ni juu yangu mimi dhifa yake. Naye hakuridhia
thawabu zozote ila pepo”. Muslim-Allah amrehemu.
Muislamu ajapo kuwa anawapendelea watu wote manufaa, lakini yeye
anawapendelea mno marafiki zake kupata manufaa. Na huzifurahikia mno
kheri wanazo zipata na wala si vibaya akipata ziada akawakumbuka
rafiki zake: “...WALA MSISAHAU FADHILA BAINA YENU. HAKIKA ALLAH
ANAYAONA MNAYO YATENDA”. [02:237]
Yaani: Na kumbukeni kuwa kheri iko katika kufadhiliana na kufanyiana
ihsani. Hayo ndio yanayo pelekea kupendana baina ya watu. Na Allah
anazijua vema dhamiri zenu na atakulipeni kwa fadhila mzitendazo.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amelipendelea suala la
kupeana hadiya (zawadi) baina ya marafiki, akasema: “Peaneni
hadiya, kwani hadiya huondosha ghushi na wasiwasi wa moyo”.
Tirmidhiy-Allah amrehemu.
Na imepokewa kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akipokea hadiya na
akiombea thawabu juu yake”. Al-Bazzaar-Allah amrehemu.
Uislamu; dini na mfumo wa maisha unao randana na umbile la
mwanaadamu, umeyafanya mahusiano ya urafiki kuwa ni njia ya
kuyarahisisha maisha na kuyapunguza magumu yake: “Mbora wa
marafiki mbele ya Allah, ni yule aliye mbora wao kwa rafiki yake. Na
mbora wa majirani mbele ya Allah, ni yule aliye mbora wao kwa jirani
yake”. Al-Haakim-Allah amrehemu.
Hakika Uislamu umemuhalalishia na kumruhusu mtu kula chakula cha
rafiki yake, kama anavyo kula chakula cha wazazi wake, ndugu zake na
jamaa zake: “...MKILA KATIKA NYUMBA ZENU, AU NYUMBA ZA BABA ZENU,
AU NYUMBA ZA MAMA ZENU, AU NYUMBA ZA KAKA ZENU, AU NYUMBA ZA DADA
ZENU...” mpaka alipo sema: “....AU ZA WALIO WASHIKIA FUNGUO ZENU,
AU RAFIKI ZENU...”. [24:61]
Wala hilo halina ajabu, kwani kifungo cha mahusiano ya kirafiki, kina
thamani kubwa na athari tukufu kiasi cha kuwa madhanio ya uokovu
katika dhiki kuu. Hata kama zingeli kuwa dhiki/shida hizo ni uokovu
kutokana na adhabu ya Jahannamu. Allah Ataadhamiaye anasema katika
wasifu wa hali ya washirikina pale watakapo onja ukali wa adhabu:
“WALLAH! KWA YAKINI TULIKUWA KATIKA UPOTOVU ULIO DHAAHIRI. TULIPO
KUFANYENI NI SAWA NA MOLA MLEZI WA WALIMWENGU WOTE. NA HAWAKUTUPOTEZA
ILA WALE WAKOSEFU. BASI HATUNA WAOMBEZI WALA RAFIKI WA DHATI”.
[26:97-101]
Na kwa kuwa mahusiano haya ya kirafiki yanafungamana na haki
kubwa/nzito, ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:
“Usisuhubiane ila na muumini na wala asile chakula chako ila
mchaMngu”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.
|